Sunday, December 30, 2012

MAGARI SABA YATEKETEA KWA MOTO DAR

MAGARI saba yameteketea kwa moto katika nyumba ya Laurence Nchimbi (61) maeneo ya Tabata Kimanga jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema kuwa moto huo ulitokea juzi majira ya saa 2:30 mchana katika eneo hilo ambapo ulidaiwa kuchangiwa na hitilafu ya umeme iliyoanzia kwenye gari T 312 BGJ Double Coaster.
Aliyataja magari mengine ni T 467 CFZ Scania, T 234 BSW Double Coaster, T 530 AWG Double Coaster, T 603 CAW Nissan Civilian, T 435 BFB Nissan Civilian na T 299 BWG Nissan Civilian ambayo yaliteketea kabisa.
Alisema kuwa hadi sasa thamani ya magari hayo bado haijafahamika ambapo moto huo ulizimwa na kikosi cha Zimamoto cha jiji wakishirikiana na wananchi wa eneo hilo na hakuna madhara zaidi kwa binadamu.
Kenyela alisema kuwa upelelezi wa tukio hilo unaendelea.
Katika tukio jingine, Kamanda Kenyela alisema kuwa, juzi majira ya saa 16:00 jioni katika eneo la Manzese Tip Top mtu aliyetambulika kwa jina la Ismaili Mgawo (50), dereva wa TANESCO alifariki baada ya kujiokoa kutokana na moto uliozuka katika hoteli ya MJ.
Kenyela alisema chanzo cha moto huo kilianzia katika chumba kilichokuwa kina kiyoyozi na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Mwananyamala.
Wakati huo huo, watu wawili wamefariki dunia jijini Dar es Salaam katika matukio tofauti likiwepo la mtoto kufa maji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englebert Kiyondo alisema tukio la kwanza lilitokea juzi majira ya saa 16:30 jioni katika eneo la Somanga –Kigamboni.
Alimtaja mtoto aliyefariki dunia kuwa ni Naima Shukuru (7) ambaye alikuwa akichota maji katika kisima chenye urefu wa futi 12, na wakati akivuta maji kwa kamba alitumbukia na kunywa maji mengi na kufariki.
Kiyondo alisema mwili wa marehemu uliopolewa na wananchi wa eneo hilo na umehifadhiwa katika hospitali ya Vijibweni huku upelelezi ukiendelea.

No comments:

Post a Comment