Sunday, December 30, 2012

CHINJACHINJA WATISHIA MAISHA MARA


HOFU imetanda kwa wananchi wa Mkoa wa Mara, kutokana na kuibuka kwa vitendo vya mauaji na kisha kukatwa vichwa kwa kile kinachodaiwa kuwa ni imani za kishirikina.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumapili, ulibaini kuwa hofu hiyo imetanda kwa wananchi wa mkoa huo na maeneo ya jirani kwa baadhi ya wanaoishi vijijini kuogopa kutembea nyakati za usiku.
Aidha, uchunguzi huo umeonesha kuwa hofu hiyo imetanda zaidi kwa wananchi wa vijiji vya Butiama ambako ndiko kumekithiri matukio ya mauaji hayo ambapo wananchi wamewapa jina wauaji hao kuwa ni makilikili.
“Siku hizi watu tunaogopa kutembea usiku kutokana na kuwepo hali hiyo ya makilikili wanaokata vichwa vya watu na kuondoka navyo,” alisema mkazi mmoja wa Kijiji cha Kasahunga wilayani Bunda, ambaye hakupenda kuandikwa jina lake.
Hata hivyo Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo ikiongozwa na mwenyekiti wake ambaye ni mkuu wa mkoa, John Tupa, inaendelea na zoezi la kuhamasisha wananchi katika Wilaya ya Butiama kuanzisha vikundi vya ulinzi katika maeneo yao, ili kukabiliana na ukatili huo.
Aidha, kamati hiyo iliwataka wananchi hao kutokupokea watu wasiowafahamu na kwamba ikibidi watoe taarifa kwenye vyombo vinavyohusika pindi wanapoona watu au mtu wanayemtilia shaka.
Tupa alitoa wito kwa wazee wa mkoa huo kutumia mikutano yao, ili kuhamasisha jamii kuachana na vitendo vya uhalifu, ikiwa ni pamoja na kuacha mambo ya imani za kishirikina kwa kuwa zinarudisha nyuma maendeleo.
Kwa siku za hivi karibuni katika Wilaya ya Butiama, yameibuka matukio ya watu wasiofahamika kuvamia watu na kuwaua na kisha kuchukuwa baadhi ya viungo vyao, ambapo tayari wanawake watatu wamekwishauawa.
Kati ya matukio hayo ni yale yaliyotokea Desemba 22, mwaka huu ambapo mwanamke mmoja, Tabu Makanya (68), mkazi wa Kijiji cha Kwikuba, Kata ya Mugango, wilayani Butiama, aliuawa na watu hao na kuchukua kichwa chake.
Hata hivyo, wananchi walipiga yowe na kuwafukuza watu hao, hali iliyowafanya wakitupe kichwa hicho ambacho walikuwa wamekibebea kwenye mfuko wa sandarusi.
Jeshi la Polisi mkoani hapa, kupitia kwa Kamanda wake (RPC), Absalom Mwakyoma, limesema kuwa linafanya msako mkali wa kuwabaini watu wanaojihusisha na unyama huo, na kwamba watu 12 wamekamatwa.

No comments:

Post a Comment