Askofu mkuu wa kanisa katoriki Tanzania Kadnal Pengo
IGP Said Mwema
WATU watano wanashikiliwa na makachero wa Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumshambulia kwa risasi Padre Ambrose Mkenda wa Parokia ya Mpendae visiwani Zanzibar.
Wakati Padre Mkenda akiuguza majereha, msaidizi wake katika parokia hiyo, Padre Peter Minja, amefariki dunia.
Kunaswa kwa watuhumiwa hao, kumefanikiwa baada ya juzi serikali kutuma makachero kutoka Bara kuungana na wenzao wa Zanzibar kufanya uchunguzi wa kina kubaini waliohusika na shambulio hilo la kinyama.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, vililiambia Tanzania Daima Jumapili kuwa, watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sasa kupisha uchunguzi, wanaendelea kuhojiwa na makachero hao visiwani Zanzibar.
Kwa mujibu wa habari hizo, watuhumiwa hao walikamatwa muda na maeneo tofauti visiwani humo, na wapelelezi hao waliobobea katika masuala ya uchunguzi wa matukio ya aina hiyo, wanaendelea kuwasaka wahusika zaidi.
“Taarifa zilizopo ni kwamba, watu watano wamekamatwa, wanahojiwa ila ni mapema mno kutaja majina yao,” alisema mtoa habari wetu.
Hata hivyo, msemaji wa polisi visiwani Zanzibar, Mohammed Mhina, alipoulizwa alisema hana taarifa hizo na kuahidi kuzitoa zitakapokamilika.
Ingawa uchunguzi wa serikali unaendelea, lakini wadadisi wa mambo ya siasa wanalihusisha tukio hilo na uhasama wa kidini.
Tukio la kushambuliwa kwa padre huyo, linafanana na lile la kumwagiwa tindikali kwa Katibu Mkuu wa Mufti Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman.
Hata hivyo katika hali ya kushangaza, hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyeshikiliwa kuhusika na tukio hilo ambalo kwa namna moja au nyingine, limekuwa likihusishwa na mitazamo tofauti ya kisiasa.
Katika siku za hivi karibuni, kumeibuka vikundi vinavyoshambulia makanisa na kuharibu mali na endapo itaendelea kuachwa hivi, hali inaweza kuwa mbaya zaidi.
Padre Mkenda alipigwa risasi na watu wasiojulikana siku ya Krismasi, nje ya nyumba yake majira ya saa 12 jioni, akitokea kanisani. Alishambuliwa akiwa ndani ya gari lake na kuanguka.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma Mohammed, alisema jana kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini wahusika walifanya uhalifu huo kwa madhumuni gani kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Sisi tunahesabu kuwa kitendo hiki ni cha kihalifu na tunawatafuta wahalifu waliofanya kitendo hiki, kwa hivyo bado ni mapema kusema kwamba kitendo hiki kimefanywa na nani kwa kuwa bado uchunguzi wetu unaendelea, na hadi sasa hakuna mtu tuliyemshika kuhusikana na tukio hili” alisema.
Wakati huo huo, Msaidizi wa Padre Mkenda, Padre Piter Minja, amefariki dunia juzi.
Padre Minja alifariki katika Hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya kuugua kwa muda mfupi na mwili wake ulitarajiwa kusafirishwa Zanzibar kwa mazishi.
No comments:
Post a Comment