AZAM FC imezunduka tena
baada ya kuichapa JKT Oljoro 1-0
kwenye Uwanja wake wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam katika
mfululizo wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni hii.
Shujaa wa Azam leo
alikuwa ni mshambuliaji wa Ivory Coast,
Kipre Herman Tcheche aliyefunga bao hilo pekee dakika ya nne kwa mkwaju
wa penalti,
baada ya Yassin Juma kuunawa mpira kwenye eneo la hatari. Katika mchezo
huo,
Azam ilimpoteza kiungo wake Himid Mao dakika ya 88 aliyelimwa kadi
nyekundu kwa
kucheza rafu.
Ushindi huo, unaifanya
Azam ifikishe pointi 24 baada ya
kucheza mechi 12 na sasa inapanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa
Ligi Kuu,
ikiizidi Simba kwa pointi moja, ambayo pia imecheza mechi 12. Yanga
yenye
pointi 26, inaendelea kuongoza ligi hiyo baada ya kucheza mechi 12 pia.
Katika mechi nyingine za
ligi hiyo, bao pekee la Daniel Lyanga
dakika ya tatu, limeipa ushindi wa 1-0 Coastal Union dhidi ya Polisi
Moro Uwanja
wa Mkwakwani, Tanga, wakati bao pekee la beki Issa Rashid dakika ya 26
limeipa
Mtibwa Sugar ushindi wa 1-0 dhidi ya JKT Ruvu, Uwanja wa Manungu,
Turiani
Morogoro.
Ligi hiyo inatarajiwa
kuendelea Jumamosi, Simba na Toto
African Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Mgambo JKT na Azam FC Uwanja wa
Mkwakwani, Tanga, African Lyon na Mtibwa Sugar Chamazi, Dar es Salaam,
Prisons
na JKT Ruvu Sokoine, Mbeya, Kagera Sugar na Polisi Morogoro, Kaitaba,
Bukoba na
JKT Oljoro na Ruvu Shooting Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Mchezo wa kukamilisha
mechi za mzunguko wa kwanza utachezwa Uwanja
wa Mkwakwani, Tanga Jumapili kati ya Yanga na Coastal Union.
No comments:
Post a Comment