JESHI la Polisi mkoani Iringa, limeendeleza usiri mkubwa wa
kumficha mtuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo
cha runinga cha Channel Ten, Daudi Mwangosi.
Ikiwa ni mara ya tatu kwa mtuhumiwa huyo, Pasificus Cleophace Simon
(23), kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi jana, ulinzi mkali
ulitawala eneo hilo, huku waandishi wakipigwa vikumbo wakizuiwa kupiga
picha.
Askari wenye sare wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) wakiwa na virungu,
silaha za moto huku wengine wakivalia kiraia, walitanda mahakamani hapo
kuhakikisha hakuna mwandishi anampiga picha mtuhumiwa huyo.
Katika patashika hiyo, mwandishi wa habari wa gazeti la Majira, Eliasa
Ally, alijikuta akipigwa na askari ambao walikuwa wakimzuia kupiga
picha.
Askari aliyempiga mwandishi huyo alitambulika kwa jina moja la
Idirisa, na hivyo tukio hilo likazidisha uhasama baina ya jeshi hilo
mkoani hapa na waandishi wa habari.
Mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani akiwa amevalia jaketi lenye
kofia iliyomfunika kichwa kizima kiasi cha sura yake kutotambulika.
Akiwa mahakamani hapo, wakili wa serikali ambaye pia ni mwendesha
mashtaka ya mtuhumiwa huyo, Lilian Ngilangwa, alimweleza Hakimu Mkazi
Mwandamizi, Dyness Lyimo, kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Lyimo aliomba kesi hiyo ihairishwe hadi Novemba 7 mwaka huu itakapotajwa tena.
Pasificus alifikishwa mahakamani hapo, akidaiwa kumuua kwa makusudi
Mwangosi wakati wa ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoa
wa Iringa, mnamo Septemba 2, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment