Habari zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kwamba walimu hao walikamatwa juzi saa 5:10 asubuhi nyumbani kwa mmoja wa watuhumiwa hao, wakiendelea na harakati za kuandaa majibu ya mtihani huo.
Akithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao, Kamanda wa Polisi wa mkoani humo, Leberatus Barlow aliwataja kuwa kuwa Kija Songoli (30), Jenfrida Edward (28), Merycelina Malisel (25) na Maliam Kateti (26) ambaye alikuwa msimamizi wa mtihani huo katika kituo hicho.
Kamanda huyo alisema mwenzao, Diana Shishangali alitoweka katika mazingira ya kutatanisha na kwamba polisi wanaendelea kumsaka ili aunganishwe na watuhumiwa wenzake kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.
Akieleza mkasa huo, Kamanda Barlow alisema walimu hao walikutwa nyumbani wa Songoli wakiwa na nakala moja ya majibu ya mtihani wa hisabati.
“Pia walikuwa na vipande kadhaa vya karatasi vikiwa tayari vimeandikwa majibu ya mtihani huo, vilivyokutwa vikiwa vimefichwa chini ya godoro,” alisema Barlow.
Alisema kuwa uchuguzi zaidi unaendelea kufanywa na kwamba mpaka sasa vimepatikana baadhi ya vielelezo ambavyo ili vipelekwe kwa wataalam, lengo likiwa ni kutambua muandiko na kumbaini aliyehusika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mary Tesha ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo naye alikiri kutokea kwa tukio hilo na kuagiza yeyote atakayekamatwa kuhusika na tukio hilo, achukuliwe hatua.
“Atakayekamatwa lazima achukuliwe hatua ili iwe fundisho kwa wengine hasa walimu wenye tabia ya kutoa majibu ya mitihani,” alisema.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo alisema hadi jana alikuwa hajapata taarifa yeyote kuhusu tukio hilo.
No comments:
Post a Comment