RAIS Jakaya Kikwete amesema hajaliuza eneo la Kigamboni lililopo jijini Dar es Salaam kwa Rais Mstaafu wa Marekani, George Bush kama baadhi ya watu wanavyodai.
Rais Kikwete alisema hayo jana wakati wa sherehe za uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Kigamboni litakalogharimu kiasi cha Sh 214.6 bilioni.
“Jamani sijaiuza Kigamboni kwa George Bush, huo ni uongo unaoenezwa na watu wachache ambao ni kama viwanda vya kuutengeneza,” alisema Rais Kikwete.
Alisema wanaoeneza uongo huo ni wale wasiopenda kuona ahadi za CCM zikitekelezwa.
“Bush aje Kigamboni kutafuta nini kwani Kigamboni kuna raslimali gani hadi ipendwe kiasi hicho na Bush,” alihoji Kikwete.
Rais Kikwete alisema Kigamboni ni eneo lililotengwa na Serikali kwa ajili ya kujenga mji mpya wa kisasa kama ilivyo miji mingine duniani.
“ Hata watalii wakija Dar es Salaam wanapita tu kwenda katika mbuga za wanyama na Mji wa Zanzibar kwa sababu hakuna vivutio vya kuwafanya wakae," alisema Kikwete.
Aliongeza," ni lazima mji kama Dar es Salaam kuwe na eneo la mfano ambalo wageni wakifika wanavutiwa."
Kikwete alisema ndiyo maana Serikali imeamua kuiendeleza Kigamboni ili uje kuwa mji mpya wa kisasa unaofanana na miji mingine duniani.
Rais Kikwete alisema mji huo utakuwa na majengo ya kisasa ambayo yatakuwa kivutio kikubwa kwa wageni wanaotembelea Tanzania.
"Wakazi wa Kigamboni msiwe na wasiwasi mtalipwa fidia mnazostahili. Serikali haina mpango wa kumdhulumu mtu yoyote," alisema.
Alisema ndiyo maana Serikali imetekeleza ahadi yake kwa kuanza ujenzi wa Daraja la Kigamboni ikiwa ni matayarisho ya mji mpya.
"Mambo haya yote tunayofanya kuboresha miundombinu ni katika kulipa hadhi eneo la Kigamboni ili liweze kufanana na miji mingine," alisema.
Alisema ujenzi wa daraja hilo ni ndoto iliyoanza tangu enzi za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, lakini haukutelezwa kwa sababu ya ukosefu wa fedha.
"Wazo la kujenga daraja hili lilikuwepo tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere, lakini ulikwama kwa sababu ya ukosefu wa fedha," alisema Kikwete.
Alisema maandalizi ya kuanza kuijenga Kigamboni yameanza baada ya kuanzisha Wakala wa Kuendeleza mji wa Kigamboni ambayo imeanza kutengewa fedha.
Watembea kwa
miguu kuvuka bure
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli alisema watembea kwa miguu na waendesha baiskeli watavuka bure katika daraja hilo, lakini wenye magari watalazimika kulipia.
"Watembea kwa miguu mtavuka bure, lakini msiende kukaa juu ya daraja kama mnavyofanya katika Daraja la Manzese, jijini Dar es Salaam, mkifanya hivyo tutawatoza," alisema Magufuli.
Aliahidi kuwalipa wananchi wa Kigamboni fidia ambao nyumba zao zitabomolewa kupisha ujenzi wa daraja hilo.
Alisema wasiwasikilize watu wasioitakia mema CCM wakasema kwamba Serikali haitawalipa fidia.
"Sasa hivi tumeanza ujenzi wa daraja kwenye bahari, hapa hatalipwa mtu fidia, tutakaanza ujenzi huo kwenye ardhi, nyumba zitakazobomolewa tutalipa fidia kwa sababu upembuzi yakinifu ulikwishafanyika," alisema Magufuli.
Alisema kwa watakaoanza ujenzi wa nyumba kwa lengo la kulipwa fidia hawatapata kwa sababu watajulikana tu.
Alizitaka kampuni zinazojenga daraja hilo kukamilisha kazi hiyo kwa muda uliopangwa ili liweze kutumika kwa ajili ya kuharakisha maendeleo.
"Tutakuwa wakali kama mtajenga daraja hili katika kiwango cha chini na hivyo kuhatarisha maisha ya wananchi," alisema.
Bosi wa NSSF
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk Ramadhani Dau alisema ujenzi wa daraja hilo unagharimiwa na mfuko huo kwa asilimia 60 huku Serikali ikitoa asilimia 40.
Alisema ujenzi huo unafanywa na kampuni za China Railways Construction Ltd na China Major Bridge Construction Ltd.
Alisema daraja hilo litakuwa na urefu wa mita 680 na litakuwa na barabara sita za magari na mbili za watembea kwa miguu na kwamba litakamilika baada ya miaka mitatu.
No comments:
Post a Comment