Monday, September 24, 2012

KINANA ANG`ATUKA CCM


       Kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),   Abdulrahaman Kinana

NI BADA YA KUWA MJUMBE NEC, KAMATI KUU KWA MIAKA 25, AZUNGUMZIA UCHAGUZI 2015, HATIMA YAKE BAADA YA SIASA 

 KADA maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahaman Kinana ametangaza kung’atuka rasmi katika siasa baada ya kukitumia chama chake kwa miaka 25 akiwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Kamati Kuu (CC) na Kamati ya Maadili. Kinana ambaye amekuwa Meneja wa Kampeni za mgombea urais wa CCM tangu mwaka 1995 ulipoanza uchaguzi wa vyama vingi, alisema kwamba baada ya kutumikia chama katika nyadhifa za juu kwa robo karne sasa, ameamua kupumzika ili kuwaachia vijana waendelee kukijenga chama hicho kikongwe nchini na barani Afrika.

 “Nimekuwa Mjumbe wa NEC kwa miaka 25, bila shaka muda huu unatosha, kwani wanaCCM wamenipa heshima ya kuwa katika vikao vya juu vya chama kwa robo karne. Sasa ni wakati wa kung’atuka, nimetoa mchango kwa kadri nilivyoweza katika vikao mbalimbali na katika shughuli nyingi,” alisema. Alisema anaamini kuachana kwake na siasa hakutakuwa na madhara kwa chama chake, kwani CCM ina hazina kubwa ya viongozi ambao wana sifa na wanaweza kuongoza chama hicho kuelekea Uchaguzi wa 2015.

 “Uongozi ni kupokezana vijiti. Wako wanaCCM wazuri, walio na uwezo mkubwa na sifa za kutosha kuongoza. Nawashukuru wanaCCM na viongozi kwa heshima waliyonipa wakati wote huu,” alisema Kinana ambaye alikuwa Meneja wa Kampeni wa Rais Benjamin Mkapa kwa vipindi viwili na Rais Jakaya Kikwete kwa vipindi viwili vya uchaguzi. Kinana alisema anajivunia kufanya kazi na marais wote wa Tanzania kuanzia Mwalimu Julius Nyerere hadi Rais Kikwete kwa uadilifu mkubwa na kuheshimiana.

 ”Ushauri wangu katika vikao umekuwa ukiheshimika sana. Nimekuwa nikiheshimiwa na uongozi wote wa CCM na hata wapinzani nao tunaheshimiana. Nimesimamia kampeni za kistaarabu na ambazo zimeleta ushindi mkubwa kwa CCM tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi,” alisema. Kinana ambaye pia alikuwa Spika wa Kwanza wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), ameshauri vijana ndani ya CCM watangulize masilahi ya taifa mbele na wasikilize wananchi. Ni muhimu washikamane, wabuni mikakati ya kusaidia kukuza uchumi kwa haraka zaidi na kuendeleza umoja na undugu wetu,” alisema. 

Ushauri wa viongozi wapya CCM Kinana alishauri viongozi wapya ambao wanatarajiwa kuchaguliwa ndani ya chama chake, iwapo wataona upungufu wake wausahihishe. “Ni matumaini yangu kuwa watakaopata uongozi wataona upungufu na watasahihisha makosa yangu,” alisema. Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2015, Kinana aliwaasa viongozi wasiwaze nani anafaa kuwa mgombea urais bali washughulikie kero za wananchi. 

 “Bado tuna kazi kubwa ya kutekeleza Ilani. Tusiwasumbue Watanzania kuwa ni nani anafaa kuwa Rais bali tushughulikie matatizo yao. Kwa sasa ajenda ya CCM ni kutekeleza ahadi zetu katika sekta zote siyo kutafuta nani atakuwa Rais 2015," alisema na kuongeza: 

"Hata wapinzani wawaeleze Watanzania yale ambao wamedhamiria kutekeleza. Kueleza upungufu wa CCM ni mtaji mdogo kwa wapinzani, ajenda kubwa ni watafanya nini? Hapa bado wana kazi kubwa. Wanapoona upungufu wasisite kutusema,” Kinana ambaye ana shahada ya uzamili katika utawala na masuala ya sera kutoka Chuo Kikuu cha Harvad nchini Marekani, alisema anatarajia kufundisha na kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD) katika moja ya vyuo vikuu vya hapa nchini.

 “Baada ya kustaafu kuna mambo mawili ambayo natarajia kufanya. La kwanza ni kuona kama naweza kufundisha. Pili kusoma katika mojawapo ya vyuo vikuu vyetu,” alisema. Mbali na nyadhifa zilizotajwa huko juu, Kinana ametumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa muda mrefu na kupanda cheo hadi kufikia Kanali. Amewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Mbunge wa Arusha Mjini. 

Nape alisema Kinana ni miongoni mwa wanasiasa waadilifu wa CCM ambao wamekitumikia chama kwa muda mrefu na kwa uaminifu wa hali ya juu. Ni kweli hajagombea, lakini kutokugombea kwake hakujafungwa milango kwa CCM kumtumia au kutumia uzoefu wake pale watakapomhitaji. Alisema "Kwa mfano Mwenyekiti wa CCM ana nafasi alizopewa kikatiba kuteua wajumbe wa NEC, huwezi kujua anaweza akamwona anafaa na akamteua," 


Chanzo: www.mwananchi.co.tz 

No comments:

Post a Comment