Tuesday, October 2, 2012

MAKETE NAKO MAMBO YALIKUWA IVI KATIKA UCHAGUZI CCM


 Mgombea uenyekiti CCM wilaya ya Makete Francis Chaula akisalimiana na mjumbe kabla ya uchaguzi nje ya ukumbi
 Msimamizi msaidizi wa uchaguzi huo Bi. Consolatha Msembele
 Wajumbe wakipiga kura
 Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Jasel Mwamwala hapa akikubali kushindwa nafasi ya uenyekiti katika uchaguzi huo
 Mwenyekiti wa sasa wa CCM wilaya ya Makete Francis Chaula

Mzimu wa kuwondoa wazee kwenye nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama cha mapinduzi (CCM) wilayani Makete umezidi kudhihirika baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo Mzee Jasel Job Mwamwala kubwagwa vibaya katika uchaguzi a kumchagua mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya wilaya

Mzee Mwamwala aliyekuwa akitetea nafasi yake ya uenyekiti aliyoishikilia kwa kipindi cha miaka mitano ameshindwa kufurukuta dhidi ya wagombea wenzake aliokuwa akichuana nao ambao ni Francis Chaula na Bibi Tabia Ilomo

Mbali na nafasi ya mwenyakiti pia kulikuwa na chaguzi za nafasi nyingine ambazo ni mjumbe wa halmashauri kuu ya taifa(NEC), wajumbe wa mkutano mkuu wa mkoa, na wajumbe wa halmashauri kuu ya wilaya

Akitangaza matokeo ya uchaguzi wa nafasi yamwenyekiti Msimamizi wauchaguzi huo Bw. Honoratus Mgaya ambaye pia ni katibu wa siasa itikadi na uenezi CCM mkoa wa Iringa na Njombe amesema Francis Chaula ameibuka kinara kwa kupata kura 791, huku Mzee Mwamwala aliyekuwa akitetea nafasi yake akipata kura 155 na Bi. Tabia Ilomo akiambulia kura 09, hivyo kumtangaza rasmi Francis Chaula kuwa mwenyekiti mpya wa CCM wilaya ya Makete

“Kabla ya kuendelea na maelezo mengine vifijo na nderemo vilitawala katika ukumbi wa shule ya sekondari Iwawa huku wajumbe wakimbeba juu Francis ha kutoka naye nje ya ukumbi pamoja na kumuimbia nyimbo mbalimbali

“jembe, jembe jembe jembe jembe ni miongoni mwa sauti za wajumbe zilisikika ukumbini hapo baada ya Francis kuwa mshindi

Hali hiyo ilidumu kwa muda hali iliyomlazimu mkurugenzi wa uchaguzi huo ambaye pia ni Katibu wa CCM wilaya ya Makete Miraji Mtaturu, kuingilia kati kwa kuwataka wajumbe hao kumrejesha ukumbini mshindi huyo kwani wasimamizi wa uchaguzi hawajamaliza kazi yao ndipo walipomrudisha

“Kwa mantiki hiyo ndugu wajumbe napenda kutangaza kwenu kuwa Francis Chaula ndiye mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi wilaya ya Makete” alisema msimamizi wa uchaguzi huo

Lakini awali kabla ya kutangaza matokeo hayo ya mwenyekiti majira ya saa 05:30 usiku yalitanguliwa na yale ya nafasi ya mjumbe wa NEC ambapo Ona Amos Nkwama aliibuka kidedea kwa kupata kura 626 akifuatiwa na Peter Mponda aliyepata kura 212 huku mwanamama Isse Malila akiambulia kura 103

Kabla ya wasimamizi hao wa uchaguzi kuondoka ukumbini hapo aliwaita mbele wagombea wote wa nafasi ya NEC kuzungumzia matokeo hayo ambapo Peter Mponda na Isse Malila walikiri kushindwa kwenye nafasi hiyo na kuahidi kumuunga mkono mshindi
“Kwa kweli hatuna kinyongo tumekubali matokeo na tunaahidi kumuunga mkono na kumpa ushirikiano mshindi wetu kwani lengo ni kukijenga chama cha mapinduzi”walisema

Mshindi wa nafasi hiyo Ona Nkwama alisema anawashukuru wajumbe kwa kumchagua na kuahidi kuwawakilisha vyema kwenye nafasi waliyompa na kuongeza kuwa hakutegemea kama angeshinda na kuahidi kutumia uwezo,akili na nguvu zake zote kuwawakilisha

Kwa upande wao wagombea wa nafasi ya mwenyekiti ambao walishindwa katika kinyang’anyiro hicho Mzee Mwamwala na Tabia Ilomo nao walikubaliana na matokeo hayo

“Ndugu yangu Francis karibu kwenye uenyekiti wa CCM, najua mengi kama mzee hivyo naahidi kukupa mbinu na ushauri wangu pale utakapouhitaji, nipo tayari kushirikiana na wewe kuiendeleza CCM, aluta kontinyua” alisema Mwamwala

“Nawashukuru wajumbe mlionopa kura 09, leo hazijatosha ila naamini kipindi kijacho zitatosha tu, tumegombea mama baba na mtoto, ila mtoto katushinda naunga mkono ushindi wake” alisema Ilomo

Akiongea na wajumbe Mwenyekiti mpya wa CCM Francis Chaula aliwapongeza wajumbe wote waliompigia na hata wasiompigia kura na kuomba ushirikiano kutoka kwao ili kupambana na changamoto zilizopo kwa lengo la kukijenga chama cha mapinduzi

Amesema wale ambao hawakumpigia kura wameonesha demokrasia kwa kumchagua kiongozi wanayemtaka na hana kinyongo na yeyote kwani wote ni wanachama wa ccm

Naye mbunge wa Makete ambaye pia ni naibu waziri wa Maji mh. Dkt Binilith Mahenge alisema ni ngumu kupata kiongozi ambaye atachaguliwa na kupendwa na kila mtu, hivyo uchaguzi umekwisha hakuna haja ya kuweka makundi na badala yake wote warudi na kuwa wamoja na kuahidi kutoa ushirikiano kwa kila aliyechaguliwa

Chaula aliahirisha mkutano huo wa uchaguzi na kulazimika kuendesha kikao cha halmashauri kuu ya wilaya kwa ajili ya kufanya uchaguzi wa kumchagua katibu wa siasa itikadi na uenezi, pamoja na katibu wa uchumi ambapo Tito Sovela alichaguliwa kuwa katibu wa siasa itikadi na uenezi na Aida Chengula kuwa Katibu wa uchumi
    KWA MSAADA WA EDDY MO BLAIZE.BLOGSPOT.COM

No comments:

Post a Comment