Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), amesema hana kinyongo wala uadui na mtu yeyote kuhusu hatua ya serikali kumweka mahabusu kwenye gereza la Kisongo kwa muda wa miezi 4 kwa kukosa dhamana.
Kauli hiyo aliitoa Jumapili hii mjini Arusha wakati akizungumza katika ibada ya kwenye Kanisa la Winners Chaple, ambapo alitoa sadaka na shukrani kwa Mungu na waumini wa kanisa hilo.
Alisema amefurahi kwa sababu Mungu alimpa likizo muhimu kwa kumpendelea kwa kuwa mbunge wa kwanza kula Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya akiwa gerezani.
“Nimeomba sana, nimewaombea sana nikiwa gerezani na sikuwa najua nina uwezo wa kuomba masaa manne ila nimemhubiri Mungu sana gerezani nimeombea taifa, viongozi, Bunge, Mahakama, Ofisi ya DPP na Rais Dk. Magufuli,” alisema.
Aliongeza “Ukweli kabisa sina adui kwenye jambo hili na sina kinyongo kwenye jambo hili, ni mara ya kwanza nilimuona mke wangu akinitetea gerezani kwa hiyo mimi nilipendelewa kuliko ninyi na hamtakaa mlie Krismasi gerezani, mkimjua Mungu alivyonibadilisha kupitia gereza mtatamani muende gerezani,”
Lema aliwaeleza waumini hao kuwa Yusuph alisema wao walimkusudia mabaya lakini Mungu alimkusudia mema huku akinukuuu andiko lake la shukrani kutoka katika Biblia kitabu cha Luka 6: 27-28 na kusema kuwa hakuna mbegu dhalimu inayopandwa itakayovuna rehema.
“Lakini nawaambia ninyi mnaonisikia wapendeni adui zenu,watendeeni mema wale ambao wanawachukia ninyi, wabarikini ambao wanawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wanawaonea ninyi,” alinukuu kitabu hicho.
**************
No comments:
Post a Comment