Baadhi ya Vyombo vya habari vya hapa nchini
hivi karibuni vilitoa taarifa kuwa, Watanzania 8
wanaodaiwa kuwa ni majasusi wa Serikali ya
Tanzania wamekamatwa nchini Malawi kwa
tuhuma za kuingia kwenye mgodi wa urani wa
Kayerekera uliopo nchini Malawi kinyume cha
sheria.
Taarifa hiyo kwa mara ya kwanza ilitolewa na
chombo cha habari cha Malawi ambacho kilidai
kuwa watu hao wametumwa na Serikali ya
Tanzania ili kuchunguza kama Serikali ya Malawi
inatengeneza silaha za nyuklia kwa kutumia
madini ya urani ya kutoka mgodi huo.
Kufuatia taarifa hizo, Wizara kupitia Ubalozi wa
Tanzania nchini Malawi ulifuatilia ili kubaini
ukweli wa tukio hilo. Baada ya kufuatilia ilibainika
kuwa ni kweli Watanzania 8 kutoka taasisi ya
CARTAS iliyo chini ya Kanisa Katoliki Songea
mkoani Ruvuma walikamatwa na vyombo vya
usalama katika Wilaya ya Karonga ambayo
inapakana na Wilaya ya Kyela.
Watanzania hao mara moja walifunguliwa kesi
kwa kutuhumiwa kufanya kosa la jinai la kuingia
eneo la mgodi bila kibali (criminal trespass).
Ubalozi uliwasiliana na Taasisi ya CARTAS
kutaka kufahamu madhumuni ya watu hao
kufanya ziara nchini Malawi. Ubalozi ulielezwa
kuwa ziara hiyo ilikuwa ni ya mafunzo ambapo
walitaka kufahamu juu ya madhara yatokanayo
na machimbo ya madini ya urani. Watanzania
hao kwa sasa wapo katika gereza kuu la Mzuzu
hadi kesi yao itakapotajwa tena tarehe 04 Januari
2017.
Ubalozi unaendelea kufanya mawasiliano na
Kanisa Katoliki Songea ili kupata maelezo zaidi
kuhusu ziara ya watu hao kwa madhumuni ya
kuyawasilisha mamlaka husika ili watuhumiwa
waweze kutolewa.
Aidha, Wizara kupitia Ubalozi umebaini kuwa
CARTAS iliruhusu watu hao kufanya ziara nchini
Malawi bila kupata kibali kutoka mamlaka husika
na bila kutoa taarifa Ofisi ya Ubalozi kuhusu ziara
hiyo.
Aidha, kipindi cha kufanya ziara hiyo nchini
Malawi hakikuwa muafaka kwa kuwa watumishi
wa Serikali ya Malawi wanakuwa katika likizo ya
mwaka kuanzia tarehe 22 Desemba hadi 03
Januari 2017. Hii inakwamisha juhudi za
kuwafuatilia watu hao ikiwa ni pamoja na
kukwama kwa maombi ya kibali cha
kuwatembelea watu hao tarehe 28 Desemba
2016.
Wizara inatoa wito kwa mara nyingine kwa taasisi
za dini, vyuo vya elimu na watu binafsi kuomba
vibali na kufuata sheria za nchi nyingine
wanapofanya ziara za mafunzo au ziara
nyinginezo ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na
ofisi za Balozi zetu kwa madhumuni ya
kufahamishwa taratibu zinazotakiwa kufuatwa
kabla ya kufanya ziara husika ili kuepuka
usumbufu unaoweza kujitokeza.
Wizara, kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini
Malawi unaendelea na jitihada za kuhakikisha
kuwa suala hilo linapatiwa ufumbuzi kwa haraka.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 29 Desemba 2016.
Thursday, December 29, 2016
Taarifa ya watanzania walio shukiwa Malawi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment