Friday, October 21, 2016

Pikipiki yaajabu dar es Salaam

Na Dotto Mwaibale
PIKIPIKI yenye namba za usajili T 684 CJZ aina
ya Fokon iliyotelekezwa kwa zaidi ya mwaka
mmoja katika kituo cha waendesha bodaboda
cha Maganga Veterinary Temeke jijini Dar es
Salaam inazua hofu kwa wananchi na hata kwa
askari polisi ambao wameshindwa kuipeleka
kituoni.
Imeelezwa kwamba pikipiki hiyo iliegeshwa katika
eneo hilo na mtu mmoja ambaye alifika nayo
akiwa akiiendesha mwishoni mwa mwaka jana.
Akizungumza jana na mtandao wa www. habari
za jamii.com mmoja wa waendesha bodaboda
wa kituo hicho ambaye hakupenda kujitambulisha
jina lake alisema pikipiki hiyo inawapa hofu
wananchi wa eneo hilo na hata waendesha
bodaboda.
"Hata sisi wenyewe tuna hofu na pikipiki hii ndio
maana tunaegesha mbalimbali na pikipiki zetu na
ndio maana sitaki kutaja jina langu" alisema
mwendesha bodaboda huyo.
Aliongeza kuwa awali baada ya pikipiki hiyo
kutelekezwa katika kituo hicho mtu yeyote
alipokuwa akiisogelea au kuigusa ilikuwa
ikijiwasha yenyewe lakini baada ya kupita mwezi
mmoja iliacha kujiwasha jambo ambalo
limeongeza hofu kwa wananchi.
Mkazi mwingine wa eneo hilo aliyejitambulisha
kwa jina moja la Ismail alisema hata walipotoa
taarifa kituo cha polisi cha Maganga walishindwa
kuichukua pikipiki hiyo kutokana na tabia ya
kujiwasha.
Alisema askari wa kituo hicho ambacho kipo mita
10 na eneo ambalo ipo pikipiki hiyo walitoa
taarifa kwa wenzao wa kituo cha Chang'ombe
ambao nao wameshindwa kuichukua na kwenda
nayo kituoni kwa ajili ya kumtambua mmiliki wa
pikipiki hiyo kupitia namba zake za usajili.
Ismail alisema inawezekana pikipiki hiyo
ilifungwa kifaa maalumu cha utambuzi iwapo
kama imeibiwa na ndio maana ilipokuwa ikiguswa
au kusogelewa inajiwasha yenyewe licha ya
baadhi ya watu wanahusisha kujiwasha kwake na
imani za ushirikina.
Imeelezwa kuwa pikipiki hiyo wakati inatelekezwa
ilikuwa katika hali ya upya lakini hivi sasa
imeanza kupoteza upya wake kwa kukosa
huduma ya matunzo.
Jitihada za mtandao huu kumpata Mwenyekiti wa
Serikali ya mtaa huo wa Maganga ili
kuzungumzia suala hilo zimeshindika baada ya
kuelekezwa alikuwa Manispaa ya Temeke
kwenye mkutano.

No comments:

Post a Comment