Thursday, October 20, 2016

Kutoka kwenye kurasa za watu maarufu

Majaribu hayana Budi Kuja
na Kyaka kya Pakano 

Nilivosikia sakata la wanafunzi wa elimu ya Juu kukosa mikopo nimeanza kupata hofu.

Nimeanza kupata hofu kwasababu nikiunganisha nukta naona hazioani vizuri. Nilimsikia na kumsoma mkuu wa nchi akiwa kwenye kampeini mwaka jana akisema kila mwanachuo mwenye sifa atapata mkopo.

"Serikali yangu haitarajii kuona mwanafunzi akifukuzwa chuo kwa kosa la kugoma kisa mkopo, bali ikitokea mgomo, watawajibisha maofisa wa Bodi ya Mikopo kwa kuchelewesha fedha.”  JPM  Kampeini za Urais Oktoba. 2015.

Lakini cha kushangaza mambo hayajawa kama ambavyo yalikuwa yameahidiwa kwenye kampeini. Mwaka mmoja kamili toka ahadi hiyo ilivyotolewa tunasikia habari tofauti juu ya mikopo ya elimu ya Juu.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba kati ya wanafunzi 88,000 walioomba mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu  66,000 wakosa mikopo. Mwananchi 20.10.2015

Mpaka sasa serikali imetoa mikopo kwa wanafunzi 11,000 tu nchi nzima na imeahidi kuongeza wanafunzi 10,500 katika awamu nyingine ili kufanya idadi kamili ya waliopewa mikopo ifikie 21,500 tu kati ya 88,000 walioomba mikopo. (Mwanahalisi Online 20.10.2016)

Kinachonitisha ni mambo mawili. La kwanza ni kuwa Mkuu aliahidi kwenye kampeini kuwa ikitokea kuna wanafunzi watakosa mikopo basi mabosi wa bodi ya mikopo wajiandae kuchukuliwa hatua kali.

Pili kutokana na wanachuo kadhaa kukosa mikopo ninaamini kabisa wanaweza wakawa wanafikiria kugoma.

KITENDO cha wanafunzi wa vyuo vikuu kunyimwa mikopo huku wachache waliopewa wakipunguziwa fedha za kujikimu kimeichukiza Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) na kuamua kuwazuia wanafunzi wa mwaka wa kwanza kusaini malipo ya fedha hizo. (Jamiiforums 20.10.2015)

Hatuwezi kukubaliana na uonevu huu, watoto wa masikini hawataweza kuendelea na masomo, wanapewa mpaka Sh. 500/= ya chakula na malazi kwa siku. Elimu ndiyo chimbuko la ukuaji wa sekta zote, lazima serikali iwekeze, kuwatelekeza wanafunzi ni kulitelekeza taifa,” Kasunzu Eliudi, Waziri wa Mikopo DARUSO,

Sasa ninapoona daliliza kugoma naona kama hawa wanataka kum-beep mheshimiwa rais. Mheshimiwa rais alishasema hajaribiwi. Hata alipokuwa anaongea UDSM siku alienda kuweka jiwe la msingi wa ujenzi wa maktaba akifafanua suala la wale wanachuo wa UDOM alisema, nanukuu “Kama (Udoma) wangegoma nilikuwa tayari kukifunga chuo hicho hata kwa miaka  mitano (Juni 2016)

Mheshimiwa alikuwa tayari kuifunga UDOM hata kwa miaka 5, sasa itakuwaje kama mwaka wa kwanza wataamua kugomea kabisa masomo ili mikopo iongezwe na wengine waliokosa wapewe? Je wanachuo watapishana na kauli au msimamo wa Rais alioutoa Singine mwezi wa nane??  Alisema, nanukuu“Sitaki nchi hii iwe ya vurugu, watakaoleta vurugu mimi nitawashughulikia kikamilifu bila huruma na wasije wakanijaribu, mimi ni tofauti sana na kama wapo watu wanaowatumia wakawaeleze vizuri, mimi sijaribiwi na wala sitajaribiwa,” alisema Rais Magufuli.

Nawaonea huruma sana wadogo zangu wanaoingia chuo mwaka huu lakini ninaona jinsi ambavyo itakuwa ngumu kwao kutumia ile njia iliyozoeleka njia ya Kunji.

Lakini nimuombe mheshimiwa Rais kuwa majaribu hayana budi kuja, na awe mvumilivu maana atakayevumilia mpaka mwisho huyo ndiye atakaye kuwa Mshindi.

Mungu Ibariki Tanzania

No comments:

Post a Comment