RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya
ya Mkinga mkoani Tanga, Emmanuel Mkumbo
siku moja baada ya kufikishwa mahakamani kwa
makosa ya usalama barabarani pamoja na
kutishia kumuua kwa bastola askari wa usalama
barabarani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais, Ikulu jana kwa vyombo vya
habari, Rais Magufuli ametengua uteuzi huo
kuanzia Oktoba 18, 2016.
“Uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
ya Wilaya ya Mkinga atakayejaza nafasi ya
Emmanuel Mkumbo utafanywa baadaye,” ilieleza
taarifa ya Ikulu.
Julai 7, mwaka huu, Rais Magufuli alifanya uteuzi
wa wakurugenzi wa halmashauri za majiji
matano, manispaa 21, miji 22 na wilaya (DC) 137
za Tanzania Bara.
Katika uteuzi huo uliotangazwa na Katibu Mkuu
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), Mussa Iyombe, kati ya
wakurugenzi wote 185 walioteuliwa, 65
wameteuliwa kutoka orodha ya wakurugenzi wa
zamani na 120 ni wakurugenzi wapya, akiwamo
Mkumbo aliyepangiwa Halmashauri ya Wilaya ya
Mkinga.
Juzi, Mkumbo (41) alipandishwa kizimbani katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro
kwa tuhuma za kumtishia kumuua kwa bastola
askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani
humo pamoja na kuvunja sheria za usalama
barabarani.
Mkumbo, ambaye ni mkazi wa Tegeta jijini Dar
es Salaam, alipandishwa kizimbani na alisomewa
mashtaka hayo na Mwendesha Mashtaka wa
Serikali, Sunday Hyera, akisaidiana na Ediga
Bantulaki mbele ya Hakimu Agripinas Kimanze.
Kwa mujibu wa waendesha mashitaka hao wa
serikali, mtuhumiwa huyo anakabiliwa na kesi
mbili, ya kwanza ikiwa ni kesi ya jinai kifungu
cha 226 ya mwaka 2016 na ya pili ni kesi ya
Usalama Barabarani Kifungu cha 222.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo
Oktoba 15, mwaka huu, eneo la Mkambarani
Wilaya ya Morogoro katika barabara kuu ya
Morogoro-Dar es Salaam wakati akiendesha gari
aina ya Toyota Pajero yenye namba za usajili T
845 CTJ.
Kosa la kwanza linalomkabiri Mkurugenzi
Mtendaji huyo ni kutishia kumuua kwa bastola
askari aliyejulikana kwa jina la Koplo Titunda,
akiwa katika majukumu yake ya kikazi na makosa
mengine ni kuendesha gari lenye namba T845
CTJ aina ya Toyota Pajero bila ya kuwa na leseni
na kuendesha gari bila bima.
Hyera alidai kuwa makosa mengine ni mwendo
kasi katika eneo lililoruhusiwa kuendesha
mwendo wa spidi 50 kwa saa, lakini alivuka na
kufikia 85, kugoma kupeleka gari kituo cha Polisi
na kuendesha bila kuwa na uangalifu barabarani.
Mtuhumiwa huyo alikana makosa hayo na
kuachiwa kwa dhamana, huku kesi yake
ikitarajiwa kufikishwa tena mahakamani hapo
Oktoba 31, mwaka huu, Hata hivyo, jitihada za
waandishi wa habari kupata picha ya mtuhumiwa
hazikufanikiwa baada ya askari kumziba
mtuhumiwa kwa koti pamoja na kofia aina ya
pama na kumuingiza katika gari aina ya Toyota
na kutokomea naye.
Wednesday, October 19, 2016
ASKARI POLISI MORO WAMPONZA MKURUGENZI MTENDAJI HALM YA WILAYA YA MKINGA TANGA KWA RAIS Magufuli
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment