Wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa timu ya
Yanga, jana wameendelea na mazoezi nchini Uturuki huku kocha wa timu
hiyo, Hans Van De Pluijm, akiendesha darasa kuwapa mbinu kali za kuwaua
wapinzani wao katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani
Afrika.
Yanga imepiga kambi katika hoteli kali ya Rui mjini Antalya, Uturuki
kujiandaa na mchezo wa kwanza wa Kundi A wa Kombe la Shirikisho Afrika
dhidi ya Mouloudia Olympique Bejaia Juni 19, mwaka huu, utakaofanyika
Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia, Algeria.
Taarifa kutoka ndani ya kambi hiyo zinadai kuwa timu hiyo inafanya
mazoezi asubuhi na jioni, huku katika muda wa ziada wachezaji wanaingia
darasani kwa ajili ya kufundishwa na walimu wao.
“Yanga ipo katika kambi makini, nia ni kuhakikisha tunafanya vizuri
katika michezo yetu ili tuweke historia kila mchezaji anaonekana yupo
vizuri wakifuata maagizo ya mwalimu.
“Hakutakua na mechi yoyote ya kirafiki labda mwalimu atake mwenyewe,” kilisema chanzo hicho kutoka Uturuki.
Wakati huo huo, beki wa kati wa timu hiyo, Vincent Bossou, anatarajia kujiunga na wenzake leo nchini Uturuki.
Bossou hakufanikiwa kuondoka na kikosi cha Yanga juzi alfajiri
kilichoelekea Uturuki, kutokana na kuchelewa kurejea nchini baada ya
mapumziko kwa madai ya kuwa na matatizo ya kifamilia.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo ilisema kuwa awali beki
huyo alitakiwa aungane na timu hiyo moja kwa moja Algeria baada ya
kumaliza matatizo yake ya kifamilia.
“Yanga pia itamkosa beki wake tegemeo wa kulia, Juma Abdul kwa wiki
mbili kwa sababu ya kuumia kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la
Shirikisho Mei 25 mwaka huu Yanga iliposhinda 3-1.
“Kutokana na tatizo hilo huenda Hassan Kessy, akachukua nafasi yake
pia mbali na Juma Abdul, wengine walioachwa ni Malimi Busungu, kipa
Benedictor Tinocco na mshambuliaji, Paul Nonga ambao hawamo kwenye
programu ya kocha wakati kinda Yussuf Mhilu hatakwenda kwa sababu jina
lake halijasajiliwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF),” kilisema chanzo
hicho.
Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, alisafiri na timu hiyo lakini
inasemekana kwamba hatacheza mechi hiyo ya kwanza ya Kundi A kwa sababu
anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa kwenye mchezo uliopita
dhidi ya Sagrada Esperanca nchini Angola.
Kiungo Salum Telela ni mchezaji pekee aliyemaliza msimu na Yanga
ambaye hakusafiri kwa sababu hajapewa mkataba mpya baada ya kumalizika
wa awali.
Timu nyingine katika Kundi A ni Medeama ya Ghana ambayo itafungua
dimba na TP Mazembe mjini Lubumbashi Juni 17, mwaka huu, mchezo ambao
utachezeshwa na marefa wa Shelisheli, Bernard Camille, Hensley Danny
Petrousse na Eldrick Adelaide.
No comments:
Post a Comment