Monday, February 8, 2016

MRAMBA, YONA,KUTUMIKIA KIFUNGO CHAO NJE.

Mramba, Yona,kutumikia kifungo chao nje.

Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona, ambao walikuwa wakitumikia kifungo cha miaka miwili jela, kuanzia leo wataanza kutumikia kifungo chao cha nje kwa kufanya usafi katika Hospitali ya Palestina, Sinza, Dar es Salaam.
Mawaziri hao walibadilishiwa adhabu ya jela na kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha nje mwishoni mwa wiki iliyopita na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kukamilika mchakato wa kufikia hatua hiyo.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha, alisema sheria ya huduma kwa jamii namba 6 kifungu namba 3(1) ya mwaka 2002 inasema mtu yeyote anayetiwa hatiani kwa kosa ambalo adhabu yake ni miaka mitatu kushuka chini, mahakama inaweza kumpa adhabu ya kutumikia jamii.
Mramba na Yona ambao baada ya rufaa walibakiwa na adhabu ya miaka miwili, walitiwa hatiani kwa kutumia madaraka vibaya na walitakiwa kumaliza kifungo Novemba 2016.
Hata hivyo, Hakimu huyo alisema Magereza walifikisha barua mahakamani hapo Desemba 5 mwaka jana, yenye kumbukumbu namba 151/DAR/3/11/223, wakipendekeza kifungo cha nje kwa mawaziri hao.
Hakimu Mkeha, alisema baada ya kuipokea barua hiyo mahakama iliamuru watu wa huduma za jamii kuchunguza kama wanastahili kupewa adhabu hiyo na walifanya hivyo na kurudisha ripoti kwamba wanastahili.

No comments:

Post a Comment