MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dk John
Magufuli, amewataka Watanzania kuwa makini wasije kudanganywa na
matapeli wa kisiasa watakaokuja na ahadi za uongo.
Akizungumza katika Uwanja wa Mashujaa mjini Mtwara jana, Dk Magufuli
alisema matapeli hao watakuja na ahadi nyingi, akawataka wananchi
wawasikilize na kuwapima kwa kauli na sifa zao kwa kuwa kuahidi ni
rahisi kuliko kutekeleza.
“Tusije tukadanganywa na matapeli wa kisiasa, wakinamama mnafahamu
matapeli wa mjini walivyo na maneno matamu. Maendeleo ni changamoto na
yataletwa na sisi Wanamtwara,” alisema.
Miongoni mwa matazamio ya Dk Magufuli ya Serikali atakayoiongoza kama
akichaguliwa kuwa rais, ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mtwara
kupitia Songea mpaka Mbambabay, baada ya kuboresha Bandari ya Mtwara na
kuwa ya kisasa kama ya Dar es Salaam.
Alisema bandari itaboreshwa ili pia iongeze ajira kwa wakazi wa mji
huo huku mizigo ya nchi za Zambia na Malawi, ikipitia mkoani humo.
Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Tano atakayoiongoza, itajielekeza
zaidi katika kukuza uchumi kwa watu. Akizungumza katika mikutano
mikubwa na midogo katika wilaya za Newala, Tandahimba na Mtwara Vijijini
kuhusu zao la korosho, Dk Magufuli alisema katika uongozi wake, lazima
korosho ilete uchumi mzuri kwa wakazi wa Mtwara.
“Mimi shahada yangu ya tatu (PHD) nimesomea korosho. Hakuna anayeweza
kunidanganya. Korosho siyo tu tunda la ndani, bali hata ganda ni uchumi
kwa kuwa linatengeneza gundi na dawa ya kuzuia kutu,” alisema Dk
Magufuli.
Alisema korosho ya Tanzania ni tofauti na korosho nyingine duniani,
kwa kuwa yenyewe huanza kuvunwa wakati maeneo mengine duniani wamemaliza
kuvuna.
Kwa mujibu wa Dk Magufuli, katika uongozi wake hataruhusu korosho
kuuzwa ghafi nje ya nchi, bali Serikali itahakikisha kunajengwa viwanda
vitakavyotumia malighafi ya korosho ili zao hilo lipande bei.
Kuhusu tatizo la stakabadhi ghalani ambalo limekuwa likilalamikiwa na
wakulima, Dk Magufuli alisema wamuachie yeye atahakikisha kero ya mfumo
huo inaondoshwa na wakulima hawadhulumiwi haki yao.
Akiwa Mtwara vijijini, alisema Tanzania imegundua gesi mkoani Mtwara,
hivyo akaahidi kuhakikisha gesi hiyo inaanza kunufaisha wakazi wa
Mtwara kabla ya kunufaisha wananchi wa mikoa mingine.
Katika hilo, alisema atasimamia ujenzi wa viwanda vikubwa, vya kati
na vidogo, ili vitoe ajira kwa vijana wa Mtwara, ambao watakuwa wamesoma
katika shule mbalimbali, ambazo kuanzia mwakani kutoka shule ya awali
mpaka kidato cha nne, itakuwa bure.
Awali kabla ya kutoa ahadi hizo na zingine nyingi katika sekta
mbalimbali, Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)
ya CCM, William Lukuvi, alisema Dk Magufuli ndiye mgombea pekee wa urais
kwa sasa aliyetembea kwa barabara umbali mrefu.
Kwa mujibu wa Lukuvi, Dk Magufuli ambaye amemaliza awamu ya kwanza ya
ziara ya kampeni katika mikoa saba, kutoka Katavi, Rukwa, Songwe,
Mbeya, Njombe, Ruvuma na kumalizia Mtwara jana kwa barabara, pia ndiye
mgombeapekee wa urais aliyechaguliwa katika mchakato bora na ulio wazi.
“Wako wanaodai kulikuwa na mizengwe wakati wa kumpata mgombea wa CCM.
Ngoja niwaambie, walikuwa wagombea 38, tukachuja mpaka wakabakia watano
na Magufuli akiwepo. Tukachuja tena katika mchakato wa wazi mpaka
watatu na Magufuli akawepo na wakati wa kumpata mmoja, ambaye ndiye
Magufuli, mchakato ulirushwa moja kwa moja na televisheni nchi
nzima.“Sasa tuwaulize wenzetu walikuwa wangapi na walimpataje huyo
mgombea wao, mbona hatukuwaona?” Alihoji na kuongeza kuwa Dk Magufuli ni
mgombea safi na hata marafiki zake si wa hovyo na watu wa hovyo
wanaogopa kumkaribia.
Lukuvi alisema kama Watanzania wanataka bora rais, basi huyo si Dk
Magufuli, lakini kama wanataka rais bora, basi kati ya wagombea wote wa
urais, hakuna aliye bora kama Dk Magufuli.
No comments:
Post a Comment