Friday, August 28, 2015

MAGUFURI MWENDO MDUNDO

 


MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli amesema analeta Tanzania mpya ambayo kila mwananchi atanufaika na utajiri uliopo huku akisisitiza kuwa kwake hakuna mnyonge kwani wote watatendewa sawa.
Pia, alisema iwapo atachaguliwa kuwa rais itakuwa marufuku serikali kukopa wananchi hasa wakulima na kwamba wale watakaouza mazao yao watalipwa hapo hapo na si kukopwa.
Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana katika mikutano ya kampeni kwa lengo la kuomba kura kwa wananchi wa Nkasi, na kwamba akichaguliwa kuwa rais atawasaidia wanyonge na kueleza kuwa hatakuwa tayari kuwa kimya wakati wananchi wanateseka.
Alisema anatambua changamoto ambayo wakulima wanakumbana nayo hususan ya kukopwa na serikali pindi wanapouza mazao yao, hivyo serikali yake haitakopa wananchi kwani yenyewe ndiyo yenye jukumu la kukopesha wananchi ili kuleta maendeleo ya Watanzania.

“Serikali yangu lazima iwe yenye kusaidia wakulima na kwamba ni marufuku serikali kukopa mazao ya wakulima. Nataka serikali yangu iwe ya kulipa fedha za wakulima keshi kwa keshi na siyo mkopo,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema haitakuwa sawa hata kidogo mkulima analima shamba, anapalilia, anaweka mbolea na wakati anapotaka kuuza kwa serikali anakopwa badala ya kupewa fedha zake huku akiahidi anataka watu waishi maisha mazuri.
“Lengo la kuomba ridhaa ya kuwa Rais wa Tanzania nataka kuleta Tanzania mpya, Tanzania ambayo itakuwa na maendeleo na bahati nzuri nafahamu shida za Watanzania.
“Nitazunguka nchi nzima kwa kutumia barabara ili niwe sehemu ya kushiriki mateso wanayoyapata wananchi na baada ya Oktoba 25, mwaka huu nikiwa Rais nianze kufanya kazi ya kuwatumikia na sitakuwa na utani na wazembe,” alisema Dk Magufuli.
Alisisitiza kuwa ili kufanikisha maendeleo, baraza lake la mawaziri ambalo ataliteua lazima liwe linajibu hoja za Watanzania na iwapo atamteua waziri kama anaona hataweza kutumikia taifa kwa kasi yake ni bora akae pembeni mapema.
Dk. Magufuli alisema anatambua changamoto ya kukosekana kwa dawa hospitalini, lakini anashangazwa kuona maduka ya pembeni ya hospitali yakiwa na dawa.
Alisema madaktari ambao wana tabia ya kuuza dawa kutoka hospitali za umma, moto wao unakuja kwani serikali yake itahakikisha inawashughulikia bila huruma maana hatakuwa na muda wa kuwavumilia.
Mgombea huyo wa CCM alisema iwapo atachaguliwa atahakikisha anaziba mianya ya ufujaji wa fedha za Watanzania na watumishi wa umma ambao wamekuwa wakila fedha hizo wajue mwisho wao unakaribia.
Alisema anazunguka kuomba kura kwa Watanzania na kazi yake kubwa baada ya hapo itakuwa ni kutekeleza yote ambayo ameahidi yeye binafsi na yaliyoko kwenye Ilani ya CCM.

Mzindakaya
Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe nchini, Chrizant Mzindakaya alisema Dk. Magufuli
ana sifa zote za kuwa rais wa awamu ya tano.
Mzindakaya alisema amekuwa katika siasa kwa miaka mingi, hivyo anawafahamu wote na
waliokimbia chama na kwa mtazamo wake Dk. Magufuli anatosha kuwa rais.
Alisema kuwa mgombea urais huyo ni mchakapakazi na mwadilifu na iwapo atakuwa rais
anaamini utawala wake utakuwa wa kuwatumikia Watanzania.
Samia
Wakati huo huo mwandishi wetu, Frank Balile anaripoti kutoka Moshi kuwa Mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan amewataka vijana na wanawake wa Jimbo la Vunjo Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro kuhakikisha wanapiga kura kwa kumchagua, Dk John Magufuli katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Marangu Mtoni wilayani Moshi Vijijini kuwa, atawapa pikipiki 30 ambazo zitawasaidia kuwaingizia kipato cha familia zao.
“Nitatoa pikipiki 30 kwa ajili ya vijana wa jimbo hili ili ziwasaidie kujikomboa kiuchumi, nafahamu mnakabiliwa na changamoto nyingi sana, niwahakikishie kuwa, mkimchagua Dk. Magufuli, mtakuwa mmejihakikishia kupata mambo mengi yatakayowasaidia kwa maendeleo yenu,” alisema.
Alisema mpango huo wa pikipiki utawekewa utaratibu mzuri ili uweze kuwanufaisha vijana wengi.
Pia, alisema kuwa atahakikisha anashirikiana vizuri na vijana, hasa wale wanaofanya biashara mpakani mwa Tanzania na Kenya eneo la Tarakea.
Mgombea mwenza huyo alisema kuwa Dk. Magufuli amejipanga vizuri kuhakikisha anawakwamua Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama, rangi na dini.
“Niwahakikishie ndugu zangu wa Vunjo, kama mkimchagua Dk. Magufuli, mtakuwa mmechagua maendeleo, kinyume cha hapo ni kilio tu. Tunaamini CCM itaibuka na ushindi wa kishindo, jitokezeni kupiga kura,” alisema.
Kabla ya mkutano wa kampeni Vunjo, mgombea mwenza huyo alitembelea Hospitali ya Huruma iliyopo wilayani Rombo na kuwataka wauguzi wazidi kujituma katika kazi zao na kupunguza vifo vya watoto na akina mama wajawazito wakati wa kujifungua.
Hassan aliwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo hilo, Colman Samora na wagombea udiwani wa kata zote za jimbo hilo.
Katika kampeni hizo, kada wa chama hicho ambaye kura zake hazikutosha Evod Mmanda, alisema kamwe hawezi kuihama CCM, badala yake atashiriki kumpigia debe aliyepitishwa na chama chao.
“Ninashangaa wale waliokosa nafasi ya kupeperusha bendera ya chama chetu wanahama, hao si wavumilivu, kilichokuwa kinatakiwa ni kujipanga na kumpigia kampeni aliyepitishwa na chama,” alisema.
Innocent
Mgombea wa ubunge wa CCM Jimbo la Vunjo, Innocent Shirima, alisema ikiwa atapewa ridhaa ya kuliongozo jimbo hilo, atahakikisha anapigania maslahi yanayopatikana Mlima Kilimanjaro yanawanufaisha vijana wa jimbo hilo.
Shirima alisema mipango yake mingine ni kuhakikisha vijana na akina mama wanapata mikopo ya kuendelezea biashara zao kwa manufaa yao na familia zao.
Alisema kwa upande wa wanafunzi wa shule za msingi, atashirikiana na wazazi jimboni humo na wadau wengine kuhakikisha wanapata mlo mmoja wa mchana wakiwa shuleni.
Chami
Mgombea ubunge Jimbo la Moshi Vijijini, Dk. Cyril Chami alisema tatizo kubwa katika jimbo lake ni barabara, hivyo alimwomba mgombea mwenza kuliangalia hilo baada ya kuingia madarakani.
“Mheshimiwa ninaomba uliangalie kwa mapana suala la barabara, huku mvua zinanyesha, magari hayapiti, wananchi wanakuwa katika shida sana,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angela Kairuki aliwataka wakazi wa Moshi kubadilika ikiwa wanataka maendeleo.
“Katika uchaguzi huu badilikeni, chagueni mgombea wa CCM, Davis Mosha ili mpate maendeleo, msikubali kudanganyika,” alisema Kairuki.
Katika hatua nyingine, Samia aliwaambia wananchi wa Manispaa ya Moshi kuwa tatizo la
umeme linaloendelea katika manispaa hiyo si mgawo wa umeme bali ni marekebisho
yanayofanywa na Tanesco na kwamba litamalizika muda si mrefu.
Akihutubia wananchi katika viwanja vya Majengo, Samia alisema tatizo hilo linatokana na
mitambo ya umeme ili kuimarisha miundombinu yake.
Kuhusu migambo wa manispaa, alisema waache kusumbua wafanyabiashara wadogo na Dk
Magufuli akiingia madarakani atalikomesha kwa kuwatengea maeneo maalumu ya biashara.
Aliwataka migambo waanze kutafuta kazi nyingine ya kufanya. “Mkurugenzi atakayekiuka
utaratibu huo atawajibishwa kwa sababu hatutaki watu waonewe,” alisema.
SHARE

No comments:

Post a Comment