Sunday, August 23, 2015

ILANI YA CHAMA CHA MAPINDUZI HII HAPA

 
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kuzindua ilani yake ya  uchaguzi leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya mikakati iliyotangazwa na ilani hiyo ni pamoja na kuinua kilimo kwa kuwaunganisha wakulima na Benki ya Maendeleo ya Kilimo iliyoanzishwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa nakala ya ilani iliyoifikia Nipashe jana, chama hicho kinatarajia kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo ili kuongeza tija lakini pia kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia na kuhakikisha upatikanaji wa ruzuku.

Kwa upande wa wafugaji ilani imeahidi watapewa dhamana ili kupata mikopo kwenye asasi za fedha, hususani vijana na wanawake watakaokuwa kwenye vyama vya ushirika vya ufugaji, bila kusahau utatuzi wa migogoro ya mipaka kati ya wakulima na wafugaji na hifadhi.
Kwenye madini ilani hiyo inaahidi kusimamia mfumo ya kukagua shughuli za migodi, kukusanya takwimu za madini.

Ilani imezungumzia utekelezaji wa sera mpya ya elimu bure kuanzia hatua za awali, shule ya msingi hadi sekondari ikiwamo kuandaa mfumo na muundo wa kutoa elimu hiyo bila malipo ili kuhakikisha kwamba uandikishwaji wa wanafunzi unaongezeka.

Kwa upande wa sekta ya maji ilani imeahidi kuimarisha upatikanaji wa maji safi mijini na vijijini lakini pia kuishirikisha sekta binafsi kutoa huduma ya uondoaji wa majitaka kwa njia ya ubia.

Kadhalika ilani imetangaza kiama cha Shirika la Tanesco kuwa kuanzia sasa litakoma kuwa mzalishaji na msambazaji pekee wa umeme na sasa sekta binafsi imeruhusiwa kushiriki katika kuzalisha, kusambaza na kuuza umeme bila kuingiliwa na shirika hilo kongwe.

ZANZIBAR
Sura ya sita ya ilani imezungumzia Zanzibar na kuahidi kuandaa sera na sheria ya mafuta na gesi asilia pamoja na kuandaa mipango ya kuwafundisha vijana kozi za fani ya mafuta na gesi.

Kadhalika itaweka mpango utakaohakikisha Wazanzibari wananufaika na kupata fursa za maendeleo kutoka sekta ya mafuta na gesi asilia ili kuondoa umaskini.

Pia ilani imeeleza mikakati ya kuhamasisha sekta binafsi kujenga viwanda vya usarifu wa mazao ili kuyaongeza thamani na ubora.
Mazao yanayotajwa ni ya mboga na matunda, nazi na karafuu kwa lengo la kukuza kipato cha wakulima na kurahisisha upatikanaji wa soko.

Ilani hiyo imeahidi kuimarisha maeneo ya hifadhi na usimamizi wa wanyapori walio katika hatari ya kutoweka kama paa nunga, kima punju na popo wa Pemba ili kuongeza idadi ya wanyama hao na kuimarisha utalii visiwani humo.

No comments:

Post a Comment