Waziri wa Fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis amejiuzulu katika kile
kinachoonekana kuwa ni mwafaka wa Waziri Mkuu Tsipras na wakopeshaji
wake baada ya kupata ushindi mkubwa katika kura ya maoni kuhusu mpango
wa mkopo
Tangazo hilo la kushangaza lililofanywa na Varoufakis limekuja wakati
viongozi wa UIaya wakiendelea kutafuta jibu baada ya wapiga kura wa
Ugiriki kusema kwa wingi “hapana” kwa hatua zaidi za kubana matumizi
zilizoitishwa na wakopeshaji ili nchi hiyo ipewe fedha za mkopo, katika
kura ya maoni ambayo huenda ikaifanya nchi hiyo kuondoka katika kanda ya
sarafu ya euro.
Varoufakis ambaye amewahi kupambana na wakopeshaji katika miezi
iliyopita, amesema anajiuzulu wadhifa huo kwa sababu lilikuwa wazo
ambalo Waziri Mkuu alihisi kuwa lingemsaidia kufikia makubaliano na
wakopeshaji.
Safaru ya euro iliimarika thamani baada ya tangazo la Varoufakis, ambalo
lilitarajiwa kuimarisha matumaini kuwa wakopeshaji wa Ugiriki – Benki
Kuu ya Ulaya, Halmashauri Kuu ya Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa –
IMF – huenda wakashawishiwa kurejea kwenye meza ya mazungumzo licha ya
uamuzi wa Ugiriki wa kupinga masharti ya mageuzi waliyoyaitisha kabla ya
kutoa fungu la mwisho la fedha za mkopo.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alitarajiwa kukutana na Rais wa
Ufaransa Francois Hollande mjini Paris pamoja na mikutano mingine ili
kutafakari athari za kura hiyo, ambayo ilikuwa ushindi kwa chama cha
siasa za mrengo wa kushoto cha Tsipras, ambaye alisisitiza kuwa
haikulenga kuipasua Ulaya.
Rais wa Umoja wa Ulaya Donald Tusk amesema mkutano wa kilele wa dharura
wa kanda ya sarafu ya euro utaandaliwa kesho. Wakati wachambuzi wakisema
kuna uwezekano mkubwa wa Ugiriki kiondoka katika kanda ya euro, mkuu wa
Halmashauri Kuu ya Ulaya Jean-Claude Juncker alitarajiwa kufanya
mazungumzo na mkuu wa Benki Kuu ya Ulaya Mario Draghi, Tusk, na mkuu wa
kundi la mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya Jeroen Dijsselbloem.
Wakati huo huo, mawaziri wa fedha wa Ujerumani na Ufaransa wanatarajiwa
kufanya mazungumzo kuanzia mjini Warsaw wakati maafisa wakuu wa fedha wa
kundi la sarafu ya euro wakikutana mjini Brussels.
Viongozi wa UIaya wametoa hisia tofauti kutokana na takwimu zilizotolewa
na wizara ya mambo ya ndani ya Ugiriki mapema leo zikionyesha matokeo
ya mwisho ya kura ya maoni kuwa asilimia 61.31 walipiga kura ya “Hapana”
na asilimia 38.69 wakasema “Ndiyo”. Asilimia 62.5 ilishiriki katika
upigaji kura huo.
Waziri wa Uchumi wa Ujerumani ambaye pia ni naibu kansela wa Ujerumani
Sigmar Gabriel ameliambia gazeti la Tagespiegiel kuwa Tsipras amevunja
madaraja kati ya Ugiriki na Ulaya. Amesema licha ya matamshi ya Tsipras,
mazungumzo mapya ya fedha za mkopo sasa ni magumu kufikiria. Uingereza
imeapa kufanya kila iwezalo kuulinda usalama wa uchumi wake kutokana na
kura hiyo ya Ugiriki.
Maelfu ya watu walikusanyika mjini Athens jana usiku kushangilia ushindi wa “Hapana“.
No comments:
Post a Comment