Sunday, July 5, 2015

UKAWA WASEMA MWENDO NI ULEULE


Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imekubaliana kuwa na msimamo wa pamoja wa kufuata nyayo za wabunge wenzao 46 waliofukuzwa bungeni na waliozuiwa kuhudhuria vikao viwili.

Kadhalika, wabunge Joseph Selasini (Rombo) na Khalifa Suleiman Khalifa (Gando), wamekana kauli ya kamati kuwa walijutia makosa yao baada ya kuhojiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, na kwamba leo watahudhuria vikao vya Bunge na kuonyesha msimamo wao.


Akizungumza mbele ya wabunge wenzao, Selasini alisema aliitwa na kuambiwa aeleze kilichotokea ndani ya Bunge, na kuulizwa kama alifanya fujo na alieleza kuwa kilichofanywa na wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ni kutaka mwongozo, taarifa na kuhusu utaratibu.


Khalifa alisema kimsingizi ni kutaka kuwagawa na kuwachonganisha jambo ambalo hawatalikubali na kwa pamoja watakwenda Bungeni ili kuonyesha kuwa walisingiziwa na Kamati hiyo.


Wakitoa tamko la pamoja nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, alisema wabunge wote waliofukuzwa wataendelea na vikao vyao kama kawaida nje ya ukumbi wa bunge na watatoa taarifa kwa waandishi kila siku.


Alisema Ukawa imeita wabunge wake toka sehemu mbalimbali nchini kufika bungeni kusimamia kanuni zinazopindishwa kuwa zinasimamiwa vyema na kwamba litakuwa jambo endelevu hadi watakapowafukuza wote ili wapitishe uuzaji wa rasilimali za Watanzania watakavyo.


" Wakati wao wanendelea na vikao vyao na sisi tutaendelea na vikao vyetu kama vya Bunge, mapambano yameanzia ndani ya Bunge wametutoa, yataendelea, hatutarudi jimboni wala nyumbani, tutakuwepo Dodoma kuendelea na shughuli zetu, wameitika kwa wingi ili kufikisha akidi ya upigaji kura lakini wameshakiuka kanuni," alisema Mnyika.


Alisema Kamati ya Nishati na Madini ni dhaifu kwa kuwa imekubali kuingiliwa na kuburuzwa na serikali, kwani katika kikao cha Aprili 12, mwaka huu, walipewa maoendekezo ya muswada na baada ya kikao nyaraka zote waliziacha kwa wataalamu wa serikali.


Alisema akiwa kama Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, hajashirikishwa katika hatua yoyote na awali alikuwa mjumbe wa kamati lakini walivyoona anazidisha kelele walimuondoa na hajawahi kupelekwa safari yoyote ya nje.

No comments:

Post a Comment