Ni nani kama Msuva? Jina hilo, Simon Happygod Msuva si geni katika medani ya michezo nchini.
Juzi, aligeuka habari ya mjini baada ya kutwaa
tuzo mbili katika hafla maalumu iliyoandaliwa na wadhamini wakuu wa Ligi
Kuu, Kampuni ya Simu za Mkononi, Vodacom.
Tuzo hizo ni ile ya mfungaji bora wa msimu wa
2014/15 sanjari na ile ya mchezaji Bora wa msimu huo uliomalizika mwezi
uliopita na timu yake, Yanga kutwaa ubingwa. Kwa kutwaa tuzo hizo,
mshambuliaji huyo wa Yanga na Taifa Stars aliweka kibindoni zaidi ya
Sh11 milioni.
Kivutio kikubwa kwenye hafla hiyo iliyofanyika
Ukumbi wa Golden Jubilee, Posta Mpya jijini Dar es Salaam, ilikuwa ni
familia ya Msuva iliyomwakilisha mchezaji huyo aliyeko Misri kwenye
kikosi cha Stars kinachoikabili Misri kesho kusaka tiketi ya kushiriki
fainali za Afrika 2017.
Wazazi wake, Happygod na Suzane ambao walipokea tuzo hiyo hawakuficha furaha yao wakati wa hafla hiyo.
Hata hivyo, alikuwa baba, Mzee Happygod ambaye
alitumia muda huo kueleza mengi kuhusu mwanaye huyo na mapenzi yake
makubwa katika soka.
Alisema kipaji cha mwanaye huyo mwenye umri wa
miaka 23, kilianzia Shule ya Msingi Lions iliyopo Magomeni jijini Dar es
Salaam, lakini kiliendelea alipokuwa Shule ya Sekondari ya Midland
iliyoko pia Dar es Salaam.
Atamba ‘Uhai Cup’, Azam, Simba
zampotezea.
Baada ya kucheza soka la mtaani kwenye timu ya
Wakati Ujao, ambayo hufanya mazoezi yake kwenye viwanja vya Chuo Kikuu
Dar es Salaam na kufanya vizuri, 2009 aliteuliwa katika timu ya
Kinondoni iliyoshiriki mashindano ya Copa Coca Cola alikoshika nafasi ya
pili kwa ufungaji.
Kutokana na kufanya kwake vizuri, Azam ilimchukua
katika timu yao ya vijana aliyoichezea kwenye mashindano ya Kombe la
Uhai 2010, ambako aliibuka mfungaji bora.
Hata hivyo, Msuva hakupata mkataba wa kuchezea
kikosi cha wakubwa cha Azam, ndipo akaangukia mikononi mwa Moro United
kabla ya kusajiliwa rasmi na Yanga anayoichezea hadi sasa.

No comments:
Post a Comment