Kituo cha Televisheni cha Azam kimefanya mabadiliko katika
utangazaji wa taarifa za habari, huku kikimuajiri Jane Shirima kuwa
mkurugenzi wa televisheni.
Kuanzia leo taarifa ya habari ya Azam TV itakuwa ikisomwa na watangazaji wawili na kutakuwa na pea tatu tofauti za watangazaji.
Naibu Mtendaji Mkuu wa Azam Televisheni, Tido
Mhando alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa wamejiandaa vilivyo
kuhakikisha kuwa mbali na studio bora wanakuwa pia na kikosi cha
wanahabari wenye uwezo mkubwa.
“Hapana shaka tunao vijana wazuri sana, lakini pia
tulihitaji waandishi wenye uwezo na ujuzi wa hali ya juu ili kuendana
na mikakati, fikara na mipango yetu ya kufanya mageuzi makubwa ya hali
ya utangazaji wa habari za televisheni nchini,” alisema Tido.
“Duniani pote vituo vingi vya televisheni na redio
vilianzishwa kwa mtindo kama huu. Kituo cha lugha ya Kiingereza cha Al
Jazeera kilipoanzishwa kiliajiri watangazaji waliobobea kutoka mashirika
kadhaa makubwa ya utangazaji duniani ikiwa ni pamoja na CNN, BBC na
NBC. Lakini pia lazima kuwepo na hadhi ya kuweza kuwavutia watu hao,”
alisema mkurugenzi huyo wa zamani wa redio Idhaa ya Kiswahili ya BBC.
Tido aliwataja baadhi ya waandishi na watangazaji
ambao wameungana na Azam TV kuwa ni Charles Hilary, Baruani Muhuza,
Ivona Kamuntu na Fatuma Almasi Nyangasa.
“Watangazaji hao sasa wataungana na wasomaji wetu
wazuri wa siku nyingi Rehema Salum na Nurdin Suleiman kukamilisha pea
tatu za wasomaji wa mtindo wa wawili wawili,” alifafanua Tido.
Tido alisema leo na kesho habari itasomwa na
Charles Hillary na Ivona Kamuntu wakati siku mbili nyingine itakuwa ni
zamu ya Baruhani Muhuza na Fatuma Nyangasa huku Rehema Salum na Nurdin
Suleiman nao wakiwa na zamu yao.
Alisema licha ya taarifa ya habari ya saa mbili
usiku pia wanatarajia hivi karibuni kuanzisha taarifa ya habari ya saa
saba mchana itakayokuwa ikiendeshwa na Zainab Chondo na Raymond
Nyamwihula.
“Mpango wote huu wa mabadiliko haya ya utangazaji
na upatikanaji wa habari wa Azam TV utakuwa unasimamiwa na kuratibiwa na
Joseph Warungu aliyekuwa Mwafrika wa kwanza kuongoza kitengo cha BBC
cha Focus on Africa,” alisema Tido.
Tido aliwataja wanahabari wengine mbao wamejiunga
na Azam TV kuwa ni Taji Liundi, Phillip Cyprian, Mwanga Kirahi na Jane
Shirima ambaye ataanza kazi leo kama mkurugenzi wa televisheni.
Wakati huohuo, Tido alisema kuanzia Jumamosi wiki
hii watazindua kipindi maalumu cha mahojiano ya kina kwa wote
waliotangaza na kuchukua fomu za kugombea nafasi ya urais. Kipindi hicho
kinachojulikana kwa jina la Funguka kitakuwa kinatangazwa kila siku
kuanzia saa moja kamili usiku.
No comments:
Post a Comment