Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, jana aliibukia
kwenye mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Jimbo la
Kawe, Dar es Salaam.
Mkutano huo ulikuwa wa uzinduzi wa kitabu cha kazi alizofanya
Mbunge wa jimbo hilo na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema
(Bawacha), Halima Mdee.
Askofu Gwajima alionekana kwenye jukwaa kuu na viongozi mbalimbali
wa Chadema, akiwamo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, katika
mkutano uliofanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, jijini
Dar es Salaam.
Miongoni mwa watu wengine maarufu waliokuwapo kwenye mkutano huo
ni mwimbaji wa nyimbo za injili, Flora Mbasha, ambaye aliimba wimbo
maalum kwa ajili ya chama hicho na ulizinduliwa jana.
Mkutano huo ulitanguliwa na maonyesho ya kikundi cha ulinzi cha
Chadema (Red Brigade) na baadaye wimbo maalum wa amani na pongezi kwa
chama hicho ulioimbwa na Mbasha na kuamsha shamrashamra kwa watu
waliohudhuria ikiwamo kupanda jukwaani kucheza.
HOTUBA YA MBOWE
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mbowe, akihutubia mamia ya wananchi wa
jimbo hilo, alisema uchaguzi wa mwaka huu ndiyo matamanio ya baba wa
Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambayo alikuwa nayo wakati wa siku
za mwisho za uhai wake.
“Mwalimu Nyerere alisema: “Watanzania wanataka mabadiliko,
wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM,” sasa wakati wa
kuyatafuta nje ya CCM umefika na Watanzania kwa kushirikiana na Ukawa
na wananchi wasio na chama lakini wana mapenzi mema na nchi wanaungana
nasi.”
Mbowe alisema baada ya kutembea nchi nzima amegundua Watanzania
wanayataka mabadiliko, wana uwezo wa kuyaleta na wako tayari kuyaleta,
utayari ambao hauipi amani CCM na kudai ndiyo maana ina haribu mfumo wa
uandikishaji wapigakura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa
mfumo wa Biometric Voters Registration,” alisema.
AIPOPOA MAWE NEC
Alisema juzi alitembelea vituo vya uandikishaji mkoani Mbeya katika
wilaya ya Rugwe Tukuyu, Kyela na alibaini Watanzania wanalala kwenye
vituo vya kujiandikisha kwa sasabu vifaa havitoshi na imefanyika hivyo
makusudi ili Watanzania wengi wasiandikishwe.
“Naomba kupitia mkutano huu nimshauri Mwenyekiti wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (Nec), Jaji Damian Lubuva, lawama utakayoipata kutokana na
BVR, CCM hawatakuwa na wewe, wanakutumia kwa sasa, kikiwaka utawekwa
kando,” alitahadharisha na kuongeza:
“Vifaa (BVR Kits) havitoshi, tunakuomba (Jaji Lubuva) utangaze
umeongeza siku za kujiandikisha na siyo siku saba ili wenye sifa
wajiandikishe.
“Nimeshuhudia kinamama wanalala vituoni kwa sababu uandikishaji umekuwa adhabu kwao,” alidai.
Mwenyekiti huyo wa Chadema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Ukawa,
alisema wapigakura wengi wanaunga mkono mabadiliko na wakijiandikisha
itakuwa ni kaburi kwa CCM na kuongeza:
“Jaji Lubuva kaburi ulilobeba ni lako mwenyewe, tunakuomba uongeze siku za kuandikisha wapiga kura.”
Mbowe alisema uchaguzi mkuu kikatiba unatakiwa kufanyika Oktoba 25,
mwaka huu na kwamba kwa sasa zimebaki siku 121 kufika siku hiyo na Nec
haijatangaza majimbo ya uchaguzi na uwakilishi pamoja na ratiba ya
uchaguzi.
“Wajiandae kisailokijia kuachia madaraka ya nchi, mnachelewesha
uandikishaji wa wapiga kura ili wengi wasijiandikishe zimebaki siku
chache utawala uliopo kwa sasa uondoke madarakani,” alisema Mbowe ambaye
hotuba yale ilikuwa inarushwa moja kwa moja na kituo cha ITV.
Kwa mujibu wa Mbowe, serikali itakayoundwa na Ukawa itaongoza taifa
katika misingi ya kurudisha utawala wa haki na sheria ili kurudisha
matumaini kwa wananchi wote.
Aidha, aliwataka watumishi wa umma kutokuwa na hofu kwani Ukawa
haingii kubadili au kufukuza mtu kazi, bali kufanya mabadiliko makubwa
kwa Watanzania na kwamba kitakachobadilika ni vyama vinavyoongoza nchi
na siyo mifumo ya utawala.
MISWADA YA HABARI
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
alisema Mswada ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari na Muswada wa
Sheria ya Haki ya Kupata Habari 2015, ikifikishwa bungeni mwaka huu,
wabunge wa Ukawa watasimamisha Bunge na hawatakubali kuipokea.
“Ndani ya Muswada wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari uhuru wa
kupata habari unataka ikifika saa mbili usiku, vyombo vyote vya habari
binafsi ni lazima vijiunge na TBC One kusikiliza na kutazama taarifa ya
habari, huu ni ukandamizaji na haikubaliki,” alisema huku akishangiliwa.
“Kupitia mkutano huu nawaambia siku serikali italeta miswada hiyo,
tutasimamisha Bunge halitaendelea kwa sababu huwezi kufanya uporaji wa
haki kwa kiasi hicho,” alisema.
Aidha, alisema Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandaoni 2015,
uliopitishwa katika Mkutano wa 19 wa Bunge una vifungu visivyofaa na
kwamba utawala utakaokuja hautaki sheria za kuminya uhuru wa watu na
kwamba kama rais amesaini zitabaki ‘kapuni’ iwapo Ukawa wataingia
madarakani.
Mbowe aliwataka wakazi wa jiji la Dar es Salaam kujiandikisha kwa
wingi ili kufanya mabadiliko nchini kwa kuwa jiji hilo ndilo lenye
wapigakura wengi.
Alisema licha ya kasi kubwa ya maendeleo na ukuaji wa jiji, lakini
wananchi wanaishi maeneo ambayo hayajapimwa kwa kuwa marais watatu
waliopita akiwamo Rais Jakaya Kikwete hawajafanya mipango miji na kwamba
Mwalimu Nyerere alifanya ya kwanza wakati jiji likiwa na wakazi 275,000
na mara ya pili likiwa na wakazi 750,00.
Mwenyekiti huyo alisema kwa kasi ya ukuaji wa jiji na mpango wa ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo kasi havilingani kabisa.
Kuhusu huduma ya majisafi na salama, alisema ni asilimia nane ya
wananchi ndiyo wanaopata maji safi na salama, asilimia 80 wanatumia maji
ya visima ikiwa ni miaka 51 ya Uhuru. Alisema jiji hilo ndiyo sehemu
pekee ambako mtu anaweza kukaa kwenye foleni kwa saa sita, jambo ambalo
linaonyesha utawala uliopo umeshindwa na nchi haiwezi kuendelea kwa kuwa
na utawala wa aina hiyo.
Mbowe alisema kuna dalili za wazi za serikali iliyopo kuchoka kwa
kuwa kwa sasa kuna migogoro mikubwa baina ya serikali na madereva, watu
wenye ulemavu, wanafunzi wa vyuo vikuu, wakulima na wafugaji.
ASKOFU GWAJIMA
Akizungumza na hadhara hiyo baada ya Mbowe kumaliza kuhutubia,
Askofu Gwajima alisema hotuba ya Mbowe ina ujumbe mzito na kwamba ana
amini aliyozungumza kaongozwa na Mwenyezi Mungu kuyazungumza kwa ajili
ya umma.
Alisema anatambua kuwa Chadema ina thamini mabadiliko na kutoa
baraka kwa chama hicho kuendelea na jitihada hizo kwa kuwa wakati wa
ukombozi umewadia.
MNYIKA: WANAWAKE JITOKEZENI KUGOMBEA
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika, aliwataka
wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali nchini katika uchaguzi
mkuu ili kuongoza mabadiliko nchini kama alivyofanya Mdee katika jimbo
hilo.
Alisema kinamama wana majukumu mengi, wanahangaika na shida katika
huduma za afya, kuhudumia familia, kupata maji na mahitaji mengine
muhimu ya familia, lakini wapo ambao wamejitokeza kwenye nafasi
mbalimbali za uongozi na kufanya vizuri.
Mbunge Mdee akihutubia umati wa wananchi waliohudhuria, alisema
alimkaribisha Mbasha Chadema na kwamba ni nyumbani kwa kuwa aliumia sana
alipomkosa ndani ya chama hicho.
Aidha, aliwakaribisha wasanii wengine kujiunga na chama hicho kwa kujitokeza hadharani kama alivyofanya Mbasha.
Mdee aliwashukuru wananchi wa Kawe kumuweka katika ramani ya
Tanzania na kwamba ni lazima kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
madarakani kwa kuwa kimeshindwa kutekeleza mahitaji ya Watanzania.
Aidha, alisema wanawake wa Tanzania wanateseka kwa kukosa huduma muhimu za kijamii ufisadi umekithiri ndani ya serikali.
No comments:
Post a Comment