
Hospitali ya Rufaa Mbeya
Watu watatu wamekufa papo hapo na wengine 28
kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Super Feo walilokuwa wakisafiria
kutoka jijini Mbeya kwenda Songea kupinduka na kutumbukia mtoni katika
kijiji cha Shamwanga Kata ya Inyara, Mbeya.
Ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa 12:50 asubuhi muda mfupi tu baada ya basi hilo kuanza safari.
Mashuhuda walisema basi hilo likiwa kwenye mwendo mkali lilitaka
kulipita lori lililokuwa mbele na wakati likiwa limeingia upande wa
kulia wa barabara, lilitokea lori lingine la kusafirisha mafuta kwa
mbele na hivyo magari hayo yakataka kugongana uso kwa uso.
Gasper Alfred, mkazi wa kijiji cha Shamwengo, alisema baada ya
basi hilo kumshinda dereva na kutumbukia mtoni, abiria waliokuwamo
walitoka wakiwa wameumia, huku watatu baadhi yao wakionekana kupoteza
maisha.
“Nililiona basi hili likijaribu kulipita lori la mbele, lakini kwa
upande wa pili likatokea lori lenye tenki la mafuta ndipo dereva wa basi
akaamua kulikwepa ili wasigongane uso kwa uso, lakini dereva alipotaka
kurudi barabarani gari lilimshinda na kutumbukia mtoni, nimeona watu
wengi wametolewa wakiwa wameumia na watatu wakiwa wamekufa,” alisema
Alfred.
Alisema kuwa miongoni mwa watu alioshuhudia wakitolewa kwenye gari
wakiwa wamekufa, mmoja wao ni mzungu wa jinsia ya kiume na wengine
wawili ni Watanzania, mmoja akiwa mwanaume na mwingine mwanamke.
Daktari wa zamu katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk. Lathan
Mwakyusa, alithibitisha kupokea miili ya marehemu watatu pamoja na
majeruhi 28 hospitalini hapo.
Dk. Mwakyusa alisema miongoni mwa majeruhi hao 28, kati yao 24
walitibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani huku wengine wanne wakilazimika
kulazwa hospitalini hapo kutokana na hali zao kuwa mbaya.
Aliwataja majeruhi wa ajali hiyo pamoja na maeneo wanayoishi kwenye
mabano kuwa ni Patric Mwakasege (Uyole), Erasto Nyoni (Iyunga), Ester
Nyange (Kilosa), Agness Mwambosyo (Kiwira), Omary Ally (Jacalanda),
Fatma Nyambi (Loleza), Tabia Sward (Kyela), Maua Ngonyani (Songwe),
Catheline Mbula (Dar es Salaam), Edson Omary (Chunya), Asukenye
Mwandanege (Tukuyu), Veronica Emmanuel (Kilosa), Emmanuel Mwandanege
(Tukuyu).
Wengine ni Charles Lwambano (Mbeya), Baraka Abiah (Airport) Patrick
Mlimbilwa (Songea), Mwangaza Shaibu (Airport), Felicia Mwalongo
(Songea), Francis Abel (Songea), Adam Raphael (Mbinga), Anuary Hemed
(Njombe), Canoe Ho (Rudewa), Petili Mbema (Songea), Fatma Abdallah
(Airport), Ginny Warley (Njombe), Cecilia Rengina (Njombe) na Ashraf
Abiah (Airport).
d
No comments:
Post a Comment