RAIS Jakaya Kikwete amesema kuna umuhimu wa asasi za kiraia, kufanya
shughuli zao kwa uwazi ili kuwapa fursa wananchi kujua shughuli
wanazofanya kwa niaba yao.
Alisema asasi hizo zina wajibu wa kuweka wazi hata taarifa za mapato
na matumizi ili kuwafanya wananchi kuwa na imani na taasisi hizo, ambazo
zina jukumu kubwa la kufanya baadhi ya shughuli kwa niaba yao.
Rais Kikwete aliyasema hayo jana, wakati akifungua Mkutano wa Kanda
ya Afrika unaohusu Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa
Uwazi (OGP), ambao ulihudhuriwa na wageni zaidi ya 200 kutoka nchi
mbalimbali.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais Kikwete alisema baadhi ya wabia
wa maendeleo, wamekuwa wakipitisha fedha za maendeleo kwenye asasi hizo,
hivyo ni muhimu asasi hizo kuwa wazi ili wananchi wajue wanavyonufaika
nazo.
“Wananchi wanapaswa kujua kinachoendelea kwa sababu hizo fedha
zimetolewa kwa ajili yao na sio kwa manufaa ya viongozi wa asasi hizi.
Dhana ya uwazi natuhusu wote, serikali na asasi za kiraia, tutakuwa
tunakosea sana kama tunadhani jukumu la uwazi ni la serikali pekee,”
alisema Rais Kikwete.
Alisema Tanzania ilikuwa nchi ya pili kuingia katika mpaka huo baada
ya kuzinduliwa mwaka 2011, lengo likiwa ni serikali kufanya shughuli
zake kwa uwazi kwani uwazi unawawezesha wananchi kujua haki zao na
kuwawajibisha watendaji wasiotimiza majukumu yao.
Alisema serikali imeundwa ili kuwahudumia wananchi na uhalali wa
kuendelea kuwepo ni kuwahudumia wananchi tofauti na hivyo itakuwa
imepoteza uhalali wake, alisema serikali imepanua uwazi na demokrasia.
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinaendesha serikali
yake kwa uwazi, ambapo hata taarifa muhimu za mapato na matumizi na
hesabu za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za serikali kuwekwa wazi.
Aidha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Kapteni George
Mkuchika alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi nane wananchi kwa Bara la
Afrika, ambapo mpango huo umesaidia juhudi za serikali katika
kuimarisha utawala bora.
Alisema mpango kazi wa awamu ya kwanza wa mwaka 2012/ 2013 na 2013/
2014, uliandaliwa na ulitekelezwa ambapo maeneo ya kipaumbele yalikuwa
ni kuboresha utoaji wa huduma katika sekta za afya, maji na elimu,
ambapo mafanikio mengi yalipatikana katika mpango kazi huo.
Alisema mpango kazi wa awamu ya pili 2014/2015 na 2015/ 2016,
umekamilika na utekelezaji wake unaendelea ambapo uanatarajiwa
kukamilika mwaka ujao.
No comments:
Post a Comment