Monday, December 16, 2013

MBOWE AKATAA KUNUNULIKA

Freeman Mbowe akihutubia Mwanza

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kuwa chama chake hakiwezi kuvumilia usaliti wa aina yoyote unaofanywa na makada na viongozi wasio waaminifu.
Sambamba na hilo, mwenyekiti huyo ametamba kuwa kamwe hawezi kununulika kwani hana njaa na hata Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinajua hivyo.
Mbowe alisema: “Bahati mbaya Mbowe sinunuliki, hela sina na sina njaa, lakini sinunuliki na nzuri zaidi katibu mkuu wetu Dk. Slaa naye hanunuliki na CCM wanalijua hili.”
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Malimbe mjini hapa, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Mwanza, Mbowe alisema CHADEMA hakitawafumbia macho viongozi au wanachama wasio waaminifu.
Ingawa Mbowe hakumtaja mtu kwa jina, lakini hotuba yake ilionyesha dhahiri kumlenga Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu aliyevuliwa uongozi, Dk. Kitila Mkumbo.
Viongozi hao hivi karibuni walivuliwa nafasi zao za uongozi na kupewa siku 14 za kujieleza kwanini wasifukuzwe uanachama kwa madai ya kukisaliti chama.
“Tumejenga chama makini kwa gharama kubwa sana na sasa kimekuwa tumaini la Watanzania, kwa hiyo hatuwezi kumvumilia mtu au watu kwa kufumbia macho wanapokwenda kinyume na misingi ya chama.
“Yaani mpo safarini ndani ya bahari au ziwa, halafu mnafika katikati ya bahari mtu au watu wanaanza kutoboa boti yetu, hivi huyo mtu utamwacha hivi hivi? Mkimuacha lazima mzame wote, hivyo lazima azame yeye,” alisema Mbowe.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema CHADEMA haitishwi wala kubabaishwa na propaganda na njia pandikizi zinazofanywa kwa kuandamana na mabango kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya CHADEMA wa hivi karibuni ambao viongozi wanaodaiwa kukisaliti chama waliadhibiwa.
Alisema kuwa hata yeye pamoja na Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa wako tayari kuvuliwa nyadhifa zao na hata kufukuzwa uanachama wakibainika wanakihujumu chama.
Kiongozi huyo wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, alisema kuongoza chama kikuu cha upinzani kama CHADEMA ni kazi kubwa na hakuna majaraibio.
Aliwaomba wanachama makini wajitokeze kugombea nafasi yoyote pale uchaguzi utakapoitishwa.

No comments:

Post a Comment