MWENYEKITI wa zamani wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Mwanza,
Clement Mabina, ameuawa kinyama na wananchi wenye hasira baada ya kumuua
kwa risasi mtoto mdogo anayekadiriwa kuwa na miaka 11.
Mabina anadaiwa kuuwa kwa kushambuliwa na mawe, visu na silaha za
jadi baada ya kutokea kutoelewana katika mzozo wa mashamba kati ya
kiongozi huyo na wananchi.
Kigogo huyo wa CCM ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kisesa wilayani
Magu mkoani hapa, aliuawa jana majira ya saa nane mchana katika msitu
mdogo wa Kanyama anaodaiwa kuumiliki.
Mashuhuda wa tukio hilo wameliambia Tanzania Daima kuwa chanzo cha
mauaji hayo ni kitendo cha Mabina kuwazuia wananchi kupita katika msitu
huo ambao unadaiwa awali yalikuwa ni mashamba yao anayodaiwa kuyapora.
Habari zinasema kuwa kiongozi huyo wa CCM alikuwa na mgogoro wa
mashamba na baadhi ya wananchi wa Kata ya Kisesa kiasi cha kuwa na
uhusiano mbaya.
Imedaiwa kuwa jana majira ya mchana Mabina aliwatuma watu wake
kufunga njia zote zinazopita katika msitu huo kutoka Kanyama kuelekea
maeneo mengine ya mji wa Kisesa.
Kitendo hicho kiliwaudhi wananchi waliolazimika kuwazuia watumishi hao wa Mabina na kuwaweka chini ya ulinzi.
Habari zimeongeza kuwa baada ya watumishi hao kuwekwa chini ya
ulinzi, walimtaarifu Mabina ambaye alikusanya idadi kubwa ya mabaunsa na
kuongozana nao akiwa na bastola.
Baada ya kufika katika msitu huo, Mabina alikutana na umati mkubwa wa
wananchi ambao walikusanyika kwa wingi kupinga kuzuiwa kupita katika
msitu huo.
Mabishano makubwa yalizuka kati ya Mabina na wananchi waliosikika
wakimlalamikia kwa kuwapora mashamba yao na kama hiyo haitoshi anawazuia
kupita katika msitu huo.
Kwa mujibu wa habari hizo, katika mabishano hayo, Mabina aliamrisha
mabaunsa wake waanze kuwashambulia wananchi hao na ndipo mapigano
yalipoanza huku wananchi wakitumia mawe.
Katika mashambulizi hayo inadaiwa Mabina alimtwanga risasi mtoto mdogo ambaye jina lake halijajulikana na kumuua.
Mauaji hayo yaliamsha hasira za wananchi walioamua kupiga yowe
lililowakusanya wananchi wengi zaidi na kuanza kumshambulia kiongozi
huyo wa CCM kwa mawe, visu mapanga na silaha za jadi.
Wingi wa watu na mashambulizi yalipozidi, Mabina alijaribu kukimbia
na mabaunsa wake, lakini mvua ya mawe ilimwandamana na hatimaye
akazidiwa nguvu na kujificha katika jumba moja bovu akiwa ameloa damu.
Wananchi hao, wengine wakiwa wamebeba mwili wa kijana aliyeuawa kwa
risasi, walizidi kumshambulia kwa mawe Mabina hadi akakata roho.
Tanzania Daima lilishuhudia mwili wa Mabina uliokuwa umeharibika na
kutapakaa damu ukiondolewa na askari polisi waliofika katika eneo la
tukio huku mke wa marehemu akilia kwa uchungu.
Katibu wa CCM M
koa wa Mwanza, Joyce Masunga alithibitisha kutokea kwa kifo cha Mabina.
“Taarifa nilizozipata ni kweli Mabina ameuawa. Nimeambiwa kabla ya
kuuawa kulizuka mabishano baina yake na kundi la watu waliokuwa eneo la
tukio, baadaye Mabina akachomoa bastola yake na kumpiga risasi mwananchi
mmoja,” alisema Mjumbe wa NEC CCM taifa, Dk. Raphael Chegeni.
Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza
ambaye pia ni Mjumbe wa NEC CCM, Bonaventura Kiswaga na mwenyekiti wa
zamani wa chama hicho Wilaya ya Nyamagana, Athumani Zebedayo nao
walikiri kupokea taarifa za kuuawa kwa Mabina.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, ambaye pia ni Ofisa Mkuu wa
Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa mkoa huo, Joseph Konyo
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea.
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Jacqueline Liana, pia alikiri kupata taarifa
za kifo hicho na kuwataka wananchi waviachie vyombo vya dola kufanya
kazi yake.
Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida, idadi kubwa ya wakazi wa
Kisesa na vitongoji vyake walionekana wakishangilia tukio la kuuawa kwa
Mabina.
Baadhi ya watu walionekana wakipiga ngoma, mabati na wengine wakiendesha pikipiki na baiskeli kwa mbwembwe.
“Bora kafa, alitunyanyasa sana kwa madaraka yake. Amepora ardhi yetu,
mashamba yetu. Sasa tutapumua,” alisema mwananchi mmoja na kuungwa
mkono na wananchi wengine.
Mabina alishindwa katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa CCM wa Mkoa
wa Mwanza na Anton Diallo katika uchaguzi wa chama hicho tawala uliokuwa
na ushindani mkali.

No comments:
Post a Comment