Arusha. Polisi mkoani Arusha, imekamata magunia mengine 30 ya
dawa za kulevya aina ya bangi kwa watu sita ambao inadaiwa ni washirika
wa polisi wawili, waliokamatwa na magunia 18 ya bangi katika maeneo ya
Himo mkoani Kilimanjaro.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas
akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema watuhumiwa hao,
walikamatwa Mei 19 saa 10 jioni katika Kijiji cha Kisimiri juu, Kata ya
Ngaramtoni wilayani Arumeru.
“Wakati askari hao, waliokamatwa mkoani
Kilimanjaro, polisi mkoani Arusha pia tulikuwa katika msako wa
kuwatafuta watuhumiwa wengine wanaoshirikiana na polisi hao, katika
biashara ya kusafirisha bangi kutoka Arumeru kupeleka nchini Kenya,”
alisema Sabas.
“Siku za karibuni tulipata taarifa kutoka kwa raia
wema kwamba kuna mtandao wa wahalifu wanaoshirikiana na baadhi ya
polisi wasiyo waaminifu,” alisema Kamanda Sabas.
“Watuhumiwa hawa walifanikiwa kukimbia kabla ya kukamatwa na kutelekeza bangi hiyo kwenye nyumba zao”alisema Sabas.
Kamanda Sabas alisema uchunguzi wa tukio hilo, ukikamilika watuhumiwa hao, watafikishwa mahakamani.
Habari zilizopatikana baadaye jana kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz kuwa askari wawili waliokamatwa juzi na magunia 18 ya bangi, watashtakiwa katika mahakama za kiraia kama wakosefu wengine.
Wakati huo huo, Kamanda Sabas jana alikiri kuwapo
taarifa ya kuuawa Watanzania watatu nchini Kenya kwa tuhuma za ujambazi
na kupatikana na bunduki ya polisi aina ya Sub Mashine Gun (SMG).
Watanzania hao,Tigiki Pasto,Steven Webo na mmoja
ametambulika kwa jina moja la Kadogoo, waliuawa Mei2, mwaka huu baada ya
kuvamia wafanyabiasha na kuwapora na kuwaua wawili.
Hata hivyo, baadaye walizingirwa na wananchi hao na kuuawa na ndipo waliipata bunduki hiyo mali ya polisi.
“Ni kweli tukio hilo lipo, ila sasa kwa kuwa
linahusisha nchi mbili, linashughulikiwa kwa taratibu nyingine za nchi
na nchi”alisema Kamanda Sabas.
Hata hivyo, alikiri pia kushikiliwa kwa polisi
wawili kwa uchunguzi kutokana na kupotea kwa silaha hiyo, kwenye ghala
la polisi Wilaya ya Ngorongoro.
No comments:
Post a Comment