Iringa. Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa
jana alipandishwa kizimbani pamoja na watu wengine 76 na kusomewa
mashtaka matatu kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi, Wilaya ya Iringa.
Mchungaji Msigwa anashtakiwa kuhusika katika
vurugu zilizotokea juzi mjini Iringa kuhusu mgogoro baina ya Halmashauri
ya Manispaa ya Iringa na wafanyabiashara kwenye eneo la Mashine Tatu.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Msigwa aliachiwa
kwa dhamana ya Sh1 milioni na wenzake 49 huku wengine 27 wakirudishwa
rumande baada ya kushindwa masharti ya dhamana.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa
Mahakama ya Wilaya ya Iringa, Godfrey Isaya, Mwendesha Mashtaka, Adolph
Maganda alisema Mchungaji Msigwa aliwashawishi watu kufanya kosa kwenye
eneo la Mashine Tatu kinyume cha sheria, kushiriki katika mkusanyiko
ambao haukuwa na kibali.
Hata hivyo, Msigwa ambaye anatetewa na Wakili wa
Kujitegemea, Basil Mkwata hakuhusishwa na shtaka jingine la kuharibu
mali kwa kukusudia, ambalo linawahusu wenzake kuanzia wa pili hadi wa
76.
Pia watuhumiwa hao wa pili hadi wa 76,
walihusishwa katika shtaka la pili la kushiriki kwenye mkusanyiko lakini
hawakujumuishwa kwenye shtaka la kwanza.Kesi hiyo imeahirishwa hadi
Juni 3, mwaka huu.
Ulinzi mkali
Mchungaji Msigwa na wenzake walifikishwa mahakamani saa saba mchana wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Mbali ya mahakamani, ulinzi pia uliimarishwa
katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Iringa ambako Mchungaji Msigwa na
wenzake walikuwa wamewekwa.
Wafuasi wa mbunge huyo walifurika kwenye kituo
hicho na baadaye kwenda mahakamani hali iliyowafanya polisi kuongeza
ulinzi wa magari yenye maji ya kuwasha.
Baada ya kuachiwa kwa dhamana saa kumi na moja
jioni, Mchungaji Msigwa alibebwa juujuu na wafuasi hao ambao
walimsindikiza kwa maandamano yaliyopita barabara mbalimbali za Iringa
hadi Ofisi za Chadema Mkoa wa Iringa eneo la Mshindo.
Mbunge huyo aliwashukuru wafuasi wake na kuwaahidi
kuwa ataendelea kutetea haki zao licha ya kufunguliwa mashtaka...
“Nitawasaidia wale wote waliobaki rumande ili kukamilisha masharti ya
dhamana.”
No comments:
Post a Comment