Sunday, May 5, 2013

SAKATA LA KUWEPO ARV'S FEKI KYELA LAPATIWA MAJIBU

SAKATA LA KUWEPO ARV'S FEKI KYELA LAPATIWA MAJIBU


Na Ibrahim Yassin,Kyela

WANANCHI wilayani Kyela,mkoa wa Mbeya wameondolewa hofu iliyotanda miongoni mwao kufuatia uvumi ulitapakaa wilayani humo kuwa dawa feki za kurefusha maisha ARV’s zimeingizwa kwa njia ya panya na kufanya wananchi hao kuingiwa na hofu ya madhara ya afya zao dhidi ya matumizi ya dawa hizo.

Hofu hiyo imeondolewa jana na kaimu mganga mkuu wa hospitali ya wilaya Kyela Apaisaria Rumisha, kwenye kikao cha kawaida cha baraza la madiwani kilichoketi jana alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na diwani wa viti maalumu ,Neema Kasunga (CCM) aliyetaka kujua ni dawa kiasi gani za ARV’s feki zilizoingia wilayani Kyela na madhara yake yakoje

Alisema kuwa baada ya kugundulika kuingia kwa dawa feki za ARV’s hapa Nchini wilaya ilichukua hatua madhubuti za kupambana na dawa hizo ili kama zimeingia Kyela zirudishwe na zisitumike kwa Wananchi

Alisema kwa bahati nzuri kwa utafiti walioufanya dawa hizo feki hazikuweza kuingia wilayani Kyela na kuwa Kyela ni salama kwa maana kuwa hakuna mtu yeyote aliyeweza kutumia dawa hizo ,hivyo hakuna madhara yoyote yaliyotokea wilayani hapa kutokana na dawa hizo

Pia katika baraza hilo madiwani kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) walitaka kupata ufafanuzi wa kutaka kujua chanzo cha kushuka kwa mapato ya halmashauri licha ya kuwapo kwa vyanzo vingi vya mapato

Akitoa hoja mbele ya baraza hilo katibu wa kamati ya madiwani wa CHADEMA Ezekiel Msyani alisema kuwa kuna makampuni manne ya kibiashara yanayonunua Cocoa,yakiwemo Masoko makubwa zaidi ya matano,Maduka pamoja na mageti ya kukusanya ushuru wa mazao unaotoka nje ya wilaya lakini mapato yaliyopo hayalingani na vyanzo hivyo vya mapato vilivyopo

Akijibu hoja hiyo mkurugenzi mtendaji wa wilaya ,Abdallah Mfaume alisema kwamba ni kweli kuna baadhi ya makampuni yanakwepa kulipa kodi hizo na wao kama halmashauri wameliona hilo ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kwa lengo la kukuza kipato cha ndani cha halmashauri

Alisema kwa utafiti walioufanya mapato mengi yanaonekana kupotea kutokana na uzembe wa watumishi wachache haidha kwa kutokuwa waaminifu na kusababisha baadhi ya makampuni kupata mwanya wa kukwepa kulipa ushuru na kuwa dawa wanayo na wanaofanya hivyo wamebainika sasa na wameanza kuwachukulia hatua ambapo kwa kuanzia wamemfikisha mahakamani aliyekua afisa mtendaji wa kata ya Ipinda ,Boniface Kayuni kwa kosa la kugushi kaboni slipu ya lisiti ya ushuru kwa lengo la kuiibia halmashauri huku wengine wakisimamishwa kazi

No comments:

Post a Comment