Mkuu wa mkoa wa Njombe Captain mstafu Asery Msangi
SERIKALI imesema wakuu wa mikoa si watumishi wa umma ila ni watumishi wa kisiasa kama ilivyo kwa wabunge.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina
Kombani, alibainisha hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la
nyongeza la Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere (CHADEMA), aliyehoji
kuhusu ajira za wakuu wa mikoa ambayo si kazi ya kitaalamu na
ikizingatiwa kuwa wengi wao walioshika nyadhifa hizo ni wastaafu.
Katika swali la msingi, mbunge huyo alitaka kujua mpango wa serikali
wa kusitisha kutoa mikataba kwa wastaafu ili wahitimu wanaotoka vyuoni
wapate ajira na kujenga nchi yao.
Akijibu swali hilo, Waziri Kombani alikiri kuwapo kwa wataalamu wengi
wanaohitimu vyuo mbalimbali nchini ambapo hupatiwa ajira kulingana na
mahitaji ya nchi na pia kwa kuzingatia uwezo wa bajeti ya serikali.
Alisema mikataba hutolewa na serikali inapoonekana ni kwa manufaa ya
umma kufanya hivyo kutokana na mahitaji makubwa katika sekta husika.
“Kifungu 12.2 cha waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 1998 kinatamka wazi
kwamba endapo utaalamu wa mtumishi unahitajika sana, serikali
inawajibika kumwomba mtumishi kuendelea kufanya kazi na si mstaafu
mwenyewe kuomba,” alisema Kombani.
Waziri Kombani alisema kwa sasa serikali inawapa mikataba wataalamu
wastaafu ambao si rahisi kuwapata katika soko la ajira, hususan
wataalamu wa kada muhimu kama vile walimu, waganga, wahandisi na
wahadhiri wa vyuo vikuu.
Alisema kutokana na kuhitaji kwao wataalamu hawa wastaafu wanaendelea
kutumiwa kwa kuwapa mikataba ya muda mfupi sambamba na kuajiri wahitimu
wa vyuo mbalimbali.
Waziri huyo alisema kwa mantiki hiyo serikali itaendelea kuajiri
wastaafu katika kada hizo muhimu hadi hapo soko la ajira
litakapojitosheleza.
No comments:
Post a Comment