TUHUMA mpya zimeibuka kuhusu tukio la uporaji wa kutumia silaha
wa sh bilioni 5.3 katika Benki ya NBC tawi la Kibo mjini hapa, uliotokea
Mei 21 mwaka 2004, ambao unadai ulipangwa na kufanikishwa kwa kiwango
kikubwa na vigogo wa Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro ambao hivi sasa
wamekuwa mabilionea.
Mmoja wa vigogo hao (jina tunalo) anadaiwa kuwa baada ya kusuka
mipango yote na kukamilika alisafiri nje ya nchi kama njia mojawapo ya
kupoteza ushahidi na mwingine akizima redio ya mawasiliano ya polisi
(radio call) na kufika eneo la tukio kwa zaidi ya saa moja baada ya
uporaji huo kutendeka.
Taarifa za siri kuhusina na tukio hilo la uporaji ambazo Tanzania
Daima Jumatano limezipata hivi karibuni, zimebainisha kuwa askari
waliokuwa lindoni na ambao walikamatwa na kufikishwa mahakamani,
waliachiwa huru na mahakama ikiwa ni mpango uliosukwa na vigogo hao wa
polisi ili kuepuka uwezekano wa kuwataja mabosi wao.
Mtoa taarifa ndani ya jeshi hilo ambaye alikuwapo wakati uporaji huo
ukitokea, ameliambia gazeti hili kwamba vigogo hao kwa sasa ni
mabilionea wakiwa na ukwasi usiomithilika ambako baadhi yao wamenunua
maeneo makubwa ya ardhi na kujenga majengo makubwa ya ghorofa katika
Jiji la Dar es Salaam.
“Wizi huo unadaiwa kupangwa kwa ustadi mkubwa kwani wezi hao waliingia
ndani ya benki kwa kupitia mlango ambao hutumiwa na wateja wakubwa na
kufanikiwa kupora kiasi hicho cha fedha bila kufyatua risasi ukiachilia
mbali kuwaweka chini ya ulinzi wateja waliokuwa ndani ya benki,”
kilieleza chanzo chetu.
Inaelezwa kwamba baada ya tukio hilo, majambazi hao waliondoka ndani
ya benki hiyo bila kupata upinzani wowote kutoka kwa askari wa Kikosi
cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliokuwa lindoni siku hiyo ya tukio na
kutokomea kusikojulikana.
Kwa mujibu wa habari, askari mmoja aliyekuwa lindoni katika benki
hiyo, aliponea chupuchupu kupigwa risasi na wenzake baada ya kutaka
kuingilia kati uporaji huo kutokana na kutokuwa mmoja wa
walioshirikishwa katika mipango hiyo.
Kutokana na hali hiyo askari huyo aliishia kusalimu amri na kuwa
miongoni mwa askari walionufaika na mgawo wa fedha zilizoporwa katika
benki hiyo baada ya askari aliyekuwa akifahamu mipango yote kutokuwapo
siku ya tukio.
Inadaiwa kuwa mmoja wa vigogo hao alihojiwa na Makao Makuu ya Polisi
jijini Dar es Salaam, lakini suala hilo lilizimwa kama njia ya kuepusha
aibu kwa kigogo huyo na inadaiwa kuwa amekuwa akienda kwa waganga wa
kienyeji kila uchao katika moja ya wilaya za Mkoa wa Tanga.
Wakati huo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro alikuwa Mohamed
Chico (sasa amestaaafu) lakini aliondolewa katika nafasi hiyo na na
kurejeshwa makao makuu ya jeshi hilo Dar es Salaam baada ya kukaa katika
nafasi hiyo kwa muda wa miaka 10.
Hata hivyo, haikuweza kufahamika mara moja ni nini kilichosababisha
jeshi hilo kufanya uamuzi huo kwa Kamanda Chico kuondolewa wadhifa wake
na kurejeshwa makao makuu ya jeshi hilo kwani hakuna taarifa za wazi
zilizoelezea sababu za hatua hiyo.
Katika tukio hilo, mfanyabiashara maarufu jijini Arusha, Jackson Ole
Nemeten ambaye kwa sasa ni miongoni mwa watuhumiwa waliopatikana na
hatia ya kufungwa jela, alikamatwa na kiasi cha sh 47.8 huku Benjamin
Julias mkazi wa Kijiji cha Nduguti Wilaya ya Iramba mkoani Singida
akikamatwa na kiasi cha sh milioni 57.5.
No comments:
Post a Comment