Rufaa hiyo imekatwa na Serikali dhidi ya Zombe aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya mauaji ya wachimba madini ya vito mkoani Morogoro.
Dar es Salaam. Rufaa ya Jamhuri
dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah
Zombe na askari wenzake wanane, sasa imepangwa kusikilizwa mwezi huu.
Awali rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa na Mahakama
ya Rufani Desemba 11, 2012, lakini ilikwama kutokana na kuugua kwa Jaji
Semistocles Kaijage ambaye alikuwa ni mmoja katika jopo la majaji
waliopangwa kuisikiliza. Majaji wengine katika jopo hilo walikuwa ni,
Jaji Nathalia Kimaro na Jaji Catherine Oriyo.
Siku hiyo Jaji Kimaro alisema kuwa wasingeweza
kuendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo kwa kuwa Jaji Kaijage anaumwa na
kwamba anaihirisha hadi Msajili wa mahakama hiyo atakapoipangia tarehe
nyingine.
Hata hivyo kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya
mahakama hiyo vya mwezi April, sasa rufaa hiyo imepangwa kusikilizwa
Aprili 22 na 23, 2013, kuanzia saa 3:00 asubuhi. Ratiba hiyo pia
inaonyesha kuwa rufaa hiyo itasikilizwa na jopo la majaji watatu tofauti
na wale wa kwanza. Majaji hao ni Edward Rutajangwa, Salum Mbarouk na
Bernard Luanda.
Zombe na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashtaka
ya mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka
Mahenge mkoani Morogoro na dereva wa teksi wa Manzese jijini Dar es
Salaam.
Hata hivyo, Agosti 17, 2009, Mahakama Kuu Kanda ya
Dar es Salaam iliwaachia huru washtakiwa wote ikisema kuwa baada ya
kusikiliza ushahidi na hoja za mawakili wa pande zote imeridhika kuwa
washtakiwa hawakuwa na hatia.
No comments:
Post a Comment