Thursday, April 18, 2013

RAIS KIKWETE NA RAIS WA ZANZIBAR DR.SHEIN WAONGOZA MAZISHI YA BI.KIDUDE



RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AONGOZA MAZISHI YA BI KIDUDE
 
 

 
Licha ya mvua kubwa iliyonyesha katika maeneo ya kijiji cha Kitumba Wilaya ya Kati, Mkoa wa kusini, Unguja, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania , Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Sheni leo mchana waliwaongoza maelfu ya Watanzania na wasanii mbali mbali katika maziko ya msanii mkongwe nchini Tanzania Fatma Bint Baraka Khamis ‘Bi. Kidude’.
 
Maziko hayo yaliyotanguliwa na sala maalum iliyofanyika baada ya swala ya adhuhuri katika msikiti wa Mwembeshauri, mjini Zanzibar  ambayo ilihudhuriwa pia na makamo wa Rais wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal na Makamo wawili wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Balozi Seif Ali Iddi na viongozi wengine kadhaa wa serikali na taasisi za sanaa nchini.

Aidha wasanii mbali mbali wakiwemo wa taarab na muziki wa kizazi kipya wa ndani na nje ya Zanzibar walihudhuria katika mazishi hayo yaliyoongozwa na Kadhi Mkuu wa Zanzibar , Sheikh Khamis Haji.
 
Mwili wa marehemu Bi Kidude uliokuwa umepakiwa katika gari maalum la polisi lenye namba PT 1891 uliongoza msafara kuelekea katika makaazi ya milele ya msanii huyo maarufu majira ya saa 7.10 mchana na kufika katika eneo la makaburi ya familia ya marehemu huyo majira ya saa 7.32 na taratibu za mazishi kusita kwa muda ili kupisha mvua kubwa iliyoanza kunyesha muda mchache baada ya msafara huo kufika katika maeneo ya Mwera kilomita chache kabla ya kufika eneo la mazishi.
 
Mbali na mvua hiyo kunyesha kwa wingi kijijini hapo bado maeneo mengi ya Zanzibar ikiwemo mjini yalikuwa makavu jambo lililotafsiriwa kuwa ni baraka hasa ikizingatiwa kuwa hakukuwa na mvua iliyonyesha kijijini hapo na katika maeneo ya karibu kwa zaidi ya siku tatu.
 
Akisoma risala kwa niaba ya serikali ya Zanzibar, mkuu wa utangazaji wa shirika la utangazaji Zanzibar, ZBC, Hassan Vuai alisema serikali inatambua mchanago wa marehemu katika kukuza sanaa ndani na nje ya nchi na kwamba inamtambua na kumuweka katika orodha ya watu maarufu wenye mchango kwa Zanzibar.
 
“Serikali ya Zanzibar inatambua mchango wa marehemu na itazikusanya kazi zake na kumbukumbu nyengine na kuziweka katika makumbusho ya taifa ili lwe urithi kwa vizazi vijavyo”, alisema Vuai.
 
Aliongeza kuwa hali hiyo haitokani na umahiri wa marehemu katika kukuza sana ya muziki wa asiia bali pia umuhimu wake kwa jamii kutokana na kuwa ni miongoni mwa matabibu wa dawa asilia aliekuwa akisafiriwa sana na jamii ya watu wa Zanzibar.
 
Akizungumza na waadshi Rais Kikwete alisema licha ya kuupokea taarifa za msiba huo kwa mshtuko alisema msiba huo ni pigo kubwa kwa wasanii wachanga ambao katika siku za karibuni walikuwa wakimshirikisha katika kazi zao.
 
“Hili si pigo kwa nchi pekee bali wasanii wachanga kwani bado naamini walikuwa wakimuhitaji kufanya nae kazi na kuchota ujuzi wake”, alisema Kikwete.
 
Awali Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alitoa ubani wa shilingi Milioni 2,000,000/- kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa familia ya marehemu na kuwataka kuelewa kuwa  jamii na waswahili wa mwambao wa Afrika Mashariki wanafahamu mchango msanii  katika fani ya muziki wa taarabu na kwamba hawatasita kuuenzi.
Alisema Zanzibar imepata sifa kubwa katika nyanja za Kimataifa kutokana na mchango wa wasanii wake kueneza sanaa ya taarabu iliyotoa  fursa kwa baadhi ya watalii na wataalamu wa sana kuitembelea Zanzibar kwa lengo la kufanya utafiti au hata kushuhudia umahiri wa wasanii waliopo akiwemo Bi. Kidude.
Makamu huyo wa Rais wa Zanzibar aliitaka Familia ya ‘Bi Kidude’ kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha msiba na kuwaeleza kwamba msiba huo sio wao peke yao .
“ Kwa kweli sisi sote tunampenda sana Bi Fatma Binti Baraka ‘Bi Kidude’ lakini tuelewe kwamba Mwenyezi Mungu anampenda zaidi na ndio maana akamuhitaji”. Alinasihi Balozi Seif.
Naye Mmoja wa wana Familia hiyo Bwana Haji Ramadhan Suwed Buda kwa niaba ya Familia ya Marehemu Bi Kidude ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mchango wake wa kuungana nao katika msiba huo.
Bwana Haji alisema hatua hiyo ya Serikali imeleta faraja kwao na kupunguza machungu ya msiba huo.
Msanii Gwiji wa sanaa ya Taarab asilia na ngoma ya Unyago, Bi Kidude aliyekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 98 hakuwahi kuzaa mtoto licha ya kuolewa mara mbili katika uhai wake.
Mwenyezi Muungu ailaze roho ya marehemu 'Bi Kidude' mahali pema peponi amin.

No comments:

Post a Comment