Tuesday, April 16, 2013

PINDA, MBOWE NGOMA NZITO DODOMA

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda 


Mvutano kuhusiana na mchakato wa kupata Katiba Mpya unaozigonganisha Serikali na Chadema ulizidi kupamba moto bungeni jana wakati wa mjadala wa kuhitimisha hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alitumia muda wake karibu wote wa saa moja kujibu maoni na kumshambulia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyoyatoa kuhusu hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Hoja za Mbowe zilizoonekana kumsumbua Pinda ni malalamiko dhidi ya Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kauli yake kwamba serikalini hakuna weledi wa kuwezesha kupanga mipango ya maendeleo.

Hata hivyo, baada ya kuhitimisha hotuba hiyo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisimama kuomba mwongozo wa Spika chini ya kanuni ya 68 (7) akidai kuwa Pinda alikuwa ametoa kauli ya uongo kuwa Chadema haikuwasilisha mapendekezo yake juu ya muundo wa Mabaraza ya Katiba, badala yake walilalamika tu kwenye mkutano wa hadhara.

Akizungumzia, Pinda alieleza kumshangaa Mbowe kwa kudai kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba haina weledi wakati kuna maprofesa na kati ya hao ni Profesa Mwesiga Baregu wa Chadema.
“Hivi kweli hawa wazee na maprofesa ni mambumbumbu kweli au ni kauli ambayo hakuipangilia. Haiwezekani kwa mjumuiko wa wazee wote waliomo mle ndani.

“Tuwatendee haki Watanzania na tusiwakatishe tamaa wazee wetu ambao wamezunguka nchi nzima na kufanya kazi kubwa, kama haya ndiyo Mbowe ametumwa basi nadhani aliteleza.”
Pinda alisema kama kuna tatizo kwenye mchakato ni kutokana na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyopitishwa na Bunge.

Wakati anazungumzia suala hilo ilisikika sauti kuwa wakati sheria hiyo inapitishwa Chadema walitoka bungeni, na Pinda alirudia, “Nasikia kuwa mlitoka bungeni.”
Pinda alisema kutakuwa na Bunge la Katiba na wabunge wote ni wajumbe, pia kwa Zanzibar kuna Baraza la Wawakilishi, hivyo Mbowe kuanza kutoa maoni hayo inaonyesha wana hofu.

“Kama Chadema wana hofu basi ni jambo lingine, nilipoisoma `speech’ (hotuba) ya Mbowe mawazo yake yanaonyesha anawaza uchaguzi wa 2015 na si kitu kingine,” alisema Pinda na kupigiwa makofi na wabunge wa CCM.
Alisema Mbowe alimtisha zaidi pale aliposema kuwa wataitisha maandamano nchi nzima kupinga suala hilo, kitu ambacho si sawa.

“Wananchi msiambiwe mwandamane, kama mnapinga basi mpinge wenyewe, kwani akili za kuambiwa inabidi uchanganye na zako,” alisema Pinda na kuongeza:

“Tume haiwezi kufanya kazi kisiri na tume haitoi taarifa kwa Rais kama ilivyodaiwa na Mbowe, bali inatoa taarifa kwa umma wote. Alichosema Rais Jakaya Kikwete ni ratiba ya tume ambayo imo kwenye sheria na ilikuwa imeshatolewa na Mwenyekiti wa Tume Jaji Joseph Warioba kwenye vyombo vya habari.”

Kuhusu suala la Mabaraza ya Katiba kukaa ki-CCM, alisema kama ni hivyo basi Bunge ndiyo lililofanya makosa kwa kuwa ndiyo lililopitisha kuwa wajumbe watapitishwa na Mkutano wa Maendeleo wa Kata (WADC).
“Bado tuna mwanya mkubwa sana huko mbele wa kurekebisha mambo haya na kufika mahala pazuri,” alisema Pinda.

Alisema kinachowatia hofu Chadema ni kuwa mikutano ya WADC ina wenyeviti wengi wa CCM, jambo alilosema ni zuri kwa kuwa ndiyo wameaminiwa na wananchi.
Pinda alisema kuwa hata hiyo Tume ya Katiba ilipotaka wadau watoe mapendekezo ya mfumo wa mabaraza hayo Chadema haikuwasilisha lakini baada ya muundo uliopo kupangwa ndipo chama hicho kilitoa maoni kwenye mkutano wa hadhara.

No comments:

Post a Comment