Tuesday, April 9, 2013

MWINGUULU AKILI KUHUSIKA NA VIDEO YA LWAKATARE

HATIMAYE Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Mwigulu Nchemba, amekiri kuhusika na video inayomwonesha Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare.
Nchemba amekuwa akitajwa na viongozi wa CHADEMA kuwa anahusika kutengeneza video hiyo, kwa kuwa aliwahi kutamba wakati akihojiwa na kituo kimoja cha televisheni kuwa anayo video inayowaonesha viongozi wa chama hicho wakipanga mauaji.
Hata hivyo, tangu Nchemba atoe kauli hiyo Januari mwaka huu, Jeshi la Polisi lilikaa kimya hadi Machi 12 lilipomkamata na kumhoji Lwakatare, siku moja baada ya video hiyo kuwekwa kwenye mtandao wa You tube na mtu anayejiita ‘Bukoba Boy’.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, Nchemba alikiri kuwa ndiye aliyeipeleka video ya Lwakatare polisi na kwamba alifanya hivyo baada ya kuripoti kuandikiwa ujumbe wa simu wa kutishiwa maisha na baadhi ya viongozi wa CHADEMA.
“Niliwapelekea mimi hiyo video polisi na wakati nasema kwenye televisheni nilikuwa tayari nimewapa. Na pale nilisema makusudi baada ya Zitto Kabwe kudai kuwa mwaka jana kulitokea mauaji mengi, ndipo nikataka kumuonesha kuwa chama chake kinahusika na mikakati hiyo,” alisema.
Alipoulizwa aliipataje video hiyo na kwanini hajahojiwa polisi ili kutoa uthibitisho wa uhalali wake, Nchemba alisema: “Kuna msamaria mwema aliniletea.”
Nchemba alipobanwa ana uhakika gani kama video hiyo ina ukweli, alijibu kuwa: “Ile huhitaji akili kubwa kutambua uhalisia wake. Suala la Lwakatare CHADEMA wakubali tu na wajitokeze hadharani kwenye makanisa na misikiti, watubu na kuomba radhi kwa umma.”
Hata hivyo katika kile kinachoweza kuongeza mashaka ya Nchemba kuhusishwa kutengeneza video hiyo, alikwenda mbali zaidi akitoa hata siri za polisi, akisimulia maelezo aliyodai kuwa ndiyo yalitolewa na Lwakatare wakati akihojiwa na polisi.
“Pale video inaonesha ni nyumbani kwake, tena jikoni na hilo amekiri katika maelezo yake polisi. Pia amekubali kuwa siku hiyo alipiga chafya kama inavyoonekana. Sasa wewe mwandishi unatetea nini wakati yeye amekiri polisi kila kitu kilichomo mle,” alisema.
Maelezo ya Nchemba yalionekana kumtia hofu mmoja wa mawakili wa Lwakatare, ambaye alikuwepo wakati wote wa mahojiano polisi, Nyaronyo Kicheere, akidai kuwa ni wazi jeshi hilo linafanya kazi ya propaganda za CCM.
“Nchemba hakuwepo wakati Lwakatare akihojiwa na hata baadhi ya wanasheria katika kesi yake ya ugaidi inayomkabili hawajui alichokisema polisi, sasa huyo amepata wapi siri za polisi kama si mchezo unachezwa?” alihoji.
Kuhusu mahusiano yake na mshtakiwa wa pili katika kesi ya Lwakatare, Ludovick Joseph, ambaye anadaiwa na baadhi ya watu kuwa ndiye aliyerekodi video hiyo, Nchemba alisema walifahamiana kupitia mtandao wa kijamii wa facebook.
Alipotakiwa kufafanua ukaribu wao hadi kufikia hatua ya kumtumia fedha kwa njia ya M-Pesa kupitia simu yake, Nchemba alisema: “Mimi nilimtumia kama ninavyowapa watu wengine hata wa CHADEMA.
“Mimi sijui kama Ludovick ndiye alirekodi video hiyo, wala sikuwahi kumtuma kufanya hivyo na fedha niliyomtumia si kwamba nilikuwa nikimlipa ujira. Kwani unaweza kumpa mtu sh 50,000 tu kwa kazi hiyo?” alihoji.
Tanzania Daima lilipotaka kufahamu kama anahusika kushirikiana na vyombo vya dola kuwarubuni baadhi ya vijana wa Makao Makuu CHADEMA kwa fedha ili watumike kutoa ushahidi wa kumwangamiza Lwakatare mahakamani, Nchemba alisema: “CHADEMA haijawahi kuongoza serikali, hivyo hawajui mikono ya serikali.”
Alipotakiwa kufafanua kikao baina yake na vijana hao kilichofanyika katika Hoteli ya Sea Cliff ya jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwezi uliopita na kisha kuwatumia fedha kwa njia ya M-Pesa, Nchemba aling’aka na kuuliza: “Hiyo Hoteli ya Sea Cliff iko wapi? Maana sipajui na sijawahi kufika.”
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Mambo ya Katiba wa CHADEMA, Tundu Lissu, alifichua njama zinazofanywa ili kutengeneza ushahidi wa uongo kwa ajili ya kuutumia katika kesi ya ugaidi inayomkabili Wilfred Lwakatare.
Lissu alidai kuwa njama hizo zinafanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama na ujasusi ili kutumia ushahidi huo mahakamani dhidi ya Lwakatare.
Alisema kuna baadhi ya vijana wa CHADEMA wa Idara ya Ulinzi na Usalama wanaopewa fedha na kuahidiwa kufundishwa namna ya kuzungumza katika kesi hiyo ya Lwakatare.
Lissu alisema kuna baadhi ya vijana wakiongozwa na Saumu Mulugu, ambaye alifukuzwa kazi CHADEMA mwanzoni mwa mwaka jana, wamepokea fedha kutoka kwa kigogo mmoja wa CCM (jina linahifadhiwa) ili kufanikisha mpango huo.
Lissu alisema hadi sasa vijana hao wameshapewa sh 400,000 ili wakubali kwenda kufundishwa jinsi ya kuzungumza mahakamani kuwa CHADEMA ni chama cha kigaidi, kwamba Lwakatare alipanga mikakati ya kigaidi.
“Awali walipewa sh 400,000, wakapewa tena sh 300,000, pia wakapewa sh 35,000 mara mbili. Na fedha zote hizi walikuwa wanapewa kwa njia ya M-Pesa,” alisema Lissu.
Alidai kuwa Saumu ndiye anayeratibu mpango wote kati ya Jeshi la Polisi na vijana hao wa CHADEMA kwa kuwarubuni kwa fedha.
Alisema vikao baina ya vijana hao wa CHADEMA na Saumu vimewahi kufanyika mara kadhaa katika moja ya hoteli maarufu nchini juu ya mambo ya kwenda kuzungumza kwenye vyombo vya habari au mahakamani kwenye kesi ya Lwakatare.
Siku moja baada ya madai ya Lissu, gazeti hili lilimnasa Saumu akiwa anawasiliana na wenzake, huku akiwatuhumu baadhi yao kuwa ndio waliovujisha siri kwa Lissu.
Vilevile alionekana akiwasiliana na kigogo mmoja wa CCM ambaye alikuwa akimwita ‘mkuu’ huku akimsomea baadhi ya taarifa zilizoandikwa magazetini jana yake kuhusu kuvuja kwa siri zao.
Saumu akiwa katika grosari karibu na baa maarufu kwa jina la Kwa Kimaro, jirani na eneo la Benki Kuu ya Damu Salama, Mchikichini jijini Dar es Salaam, alisikika akiwalalamikia wenzake kwa kumsaliti na kuvujisha mkakati wao kwa Lissu.
“Kwanini mmelikisha siri zetu kwa Lissu hadi amejua tulikutana katika hoteli ya kifahari na Mwigu…? Sasa nitawaonesha, maana laki tano zenu ninazo mimi. Siwapi bali nitazitumia kujilinda,” alitamba.
Saumu ambaye alikuwa akizungumza kwa sauti kubwa ya ghadhabu kupitia simu, aling’aka: “Nyie kwanini mmeniuza kwenye ishu ambayo tumeipanga wote?”
Baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa ‘mkuu wake’ aliendelea kupiga simu akimlalamikia mtu ambaye hakumtaja, kuwa alikuwa amezima simu yake makusudi kwa kuwa ndiye alivujisha siri zao kwa CHADEMA.
“Mimi sitakubali na nimehakikishiwa na bosi wetu kuwa huyo aliyetusaliti tutatumia wale askari kumwekea hata unga. Haiwezekani fedha tumepokea za kwanza, za pili na tatu kwanini tuuzane dakika za mwisho?” alidai Saumu huku akiendelea kugida bia yake.
Huku akihaha huku na kule, Saumu alikuwa akiwapigia simu baadhi ya madereva wa CHADEMA makao makuu na kuwaomba simu za baadhi ya watu, na hata wakati mwingine kuwafokea akidai ndio waliofichua siri hiyo.
Hata hivyo, baada ya kutilia shaka nyendo za chanzo chetu kudaka siri zake, ghafla alitokomea na kuzima simu zake mara moja kwani hata alipotafutwa baadaye hakupatikana hadi leo.
Polisi wafanya unyama
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi nchini limemkamata kada wa CHADEMA mjini Bukoba, Evodius Justinian na kumshikilia kwa siku kadhaa kisha kumsafirisha hadi jijini Dar es Salaam huku akipewa mateso makali ya kulazimishwa akubali kutengeneza video ya Lwakatare.
Justinian (30), ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) mjini Bukoba, alikamatwa Jumanne ya wiki iliyopita akidaiwa kukabiliwa na makosa ya jinai.
Alishikiliwa kwa siku mbili mfululizo kabla ya kumsafirisha kwenda wilayani Igunga, Tabora ambako alidaiwa kuwa alitenda makosa hayo ya jinai lakini alifichwa jijini Mwanza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi hakutaka kulizungumzia kwa undani suala hilo lakini aligusia kuwa alikuwa anakabiliwa na mashitaka ya kushambulia na kujeruhi mtu huko wilayani Igunga.
Hata hivyo, kada huyo alisafirishwa hadi uwanja wa ndege wa jijini hapa juzi, lakini akanyang’anywa simu na kukatazwa kuzungumza na ndugu zake.
Taarifa za kada huyo kuletwa jijini hapa zilikuwa za kificho kwani wakili wake Nyaronyo Kicheere akiongozana na ndugu wa mtuhumiwa huyo walifika Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na kuelezwa kuwa amepelekwa makao makuu.
Walipofika makao makuu kumwona na kumpatia chakula, polisi walisema hawana mtu kama huyo, hivyo wakarudi tena Kanda Maalumu walipohakikishiwa kuwa yuko makao makuu.
Akizungumza mbele ya wakili wake, Kicheere, mtuhumiwa huyo alieleza unyama aliofanyiwa na jeshi hilo wakati wote wa mahojiano mkoani Mwanza na jijini hapa.
Katika maelezo yake yaliyoshuhudiwa na Ofisa wa Polisi Makao Makuu, Advocate Nyombi, Justinian alisema kuwa baada ya kutolewa mjini Bukoba kwa siri bila ndugu zake kujua, alipelekwa jijini Mwanza na kuhojiwa bila kuruhusiwa kuonana na wakili wake.
Alieleza kuwa wakati wote wa mahojiano hayo alikuwa akilazimishwa kukiri kurekodi video ya Lwakatare inayoonesha mikakati ya ugaidi.
Alisema alisafirishwa kwa siri kwa ndege hadi Dar es Salaam, akapelekwa chooni na kumpiga, kutishiwa na kuteswa kwa nyaya za umeme na kumnyima fursa ya kupewa chakula.
Justinian ambaye anaendelea kushikiliwa na polisi, anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo.
Kabla ya maelezo hayo, Kicheere akiwa na Uloleulole Juma Athumani, ambaye ni ndugu wa Justinian, alijitambulisha kwa Nyombi akimweleza kuwa walikuja kuonana na mteja wake pamoja na kumletea chakula.
Hata hivyo, Nyombi alisema hakuwa na habari za kukamatwa kwa kada huyo na kwamba angekuwa amelimaliza mapema suala hilo.
Kada huyo alisimulia unyama aliofanyiwa akisema: “Nimepigwa na polisi nikiwa Mwanza, nikiwa chooni Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam wakati naletwa huku, polisi wakaniambia mimi ni mtu hatari sana, niseme nilifanya nini Igunga.
“Nikiwa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam niliomba kwenda chooni, waliingia pamoja na mimi wakanipiga sana, nimeshaandika maelezo kwa kulazimishwa, niliomba kuwa na wakili wakanikatalia,” alisema.
Aliongeza kuwa akiwa Dar es Salaam alihojiwa aseme ukweli kuhusu video ya Lwakatare. Akawajibu kuwa ilifanyiwa uhariri na Ludovick lakini akapigwa makofi na askari wakaagiza nyaya za umeme za kutesea.
“Waliposimama kuleta nyaya za umeme, kwa kuhofia mateso ya umeme nikasema hii video ni yangu. Ninaumwa sana tumbo la kuhara damu, natumia dawa nilizonunuliwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Kagera tarehe 4 Aprili,” alisema.
Justinian aliongeza kuwa hakula chakula chochote cha polisi kwa kuwa hawaamini, ila kuhara kulipozidi alikubali kula chakula chao.
Wakili Kicheere alisema ni makosa makubwa sana kumtesa mtu kwa kipigo na vitisho vya umeme na kwamba hayakubaliki hata mahakamani.
“Polisi hawakutaka nionane naye kwa makusudi hadi walipomaliza kumhoji na kumtesa ndipo wakaniruhusu,” alisema.  http://www.freemedia.co.tz

No comments:

Post a Comment