Wednesday, April 24, 2013

MTALII AIBIWA HOTELINI DAR

RAIA wa Afrika Kusini, Henry Cocroft, ameibiwa dola za Marekani 700 akiwa katika Hoteli ya kitalii ya Giraffe ya jijini Dar es Salaam alikopanga.

Meneja wa Huduma za Jamii wa NHC, Muungano Saguya, alilieleza gazeti hili kuwa Cocroft aliwasili nchini Aprili 14 mwaka huu, kwa ajili ya kuwafundisha vijana 35 kutoka katika chuo cha Veta, namna ya kutengeneza matofali bora kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu zinazojengwa na shirika hilo.

Saguya alisema kuwa baada ya kuwasili walimpangishia chumba katika Hoteli ya Giraffe kuanzia tarehe hiyo hadi juzi alipokumbwa na kadhia hiyo.

“Huyu ni mtaalamu wa utengenezaji wa matofali bora na amepata tatizo katika hoteli ile, cha ajabu anasema wenye hoteli hawampi ushirikiano zaidi ya kumuambia kuwa wameshamfukuza meneja wa hoteli,” alisema.

Baada ya gazeti hili kufika hotelini hapo, uongozi ulionekana kuhamaki na kuhoji nani kaita vyombo vya habari.
Mmoja wa wafanyakazi wa hoteli hiyo wa idara ya mapokezi aliyejitambulisha kwa jina la Lily, alisema kuwa suala hilo linashughulikiwa kiofisi.
Alisema kuwa wanalifanyia uchunguzi ikiwa ni pamoja na kupitia kumbukumbu za kwenye kamera kuweza kubaini madai hayo kama yana ukweli.
Alipoulizwa kama wametoa taarifa polisi, Lily alitaka maswali hayo yajibiwe na meneja mkuu aliyemtaja kwa jina moja la Nicholaus.
“Nimeongea na bosi, lakini si msemaji tafadhali ungekuja kesho asubuhi utakuta tumeshajadili kila kitu na kukupa taarifa rasmi,” alisema.
Alipoulizwa kama kuna mfanyakazi aliyewajibishwa kwa tukio hilo, hakuweza kujibu na badala yake alinyanyua simu na kumpigia mtu aliyemtaja kwa jina la Muganyizi huku akimuulizia kama ndiye aliyetoa taarifa hizo kwa mwandishi wa habari na kisha kuendelea kushutumu kuwa ni mipango ya kuchafua jina la heoteli yao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alipoulizwa kama ana taarifa za tukio la raia huyo kuibiwa alisema hajazipata na kwamba atafuatilia.

No comments:

Post a Comment