ASKARI Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani
Kilimanjaro wanaolinda mipaka kukabiliana na biashara za
magendo zisiende Kenya, wanadaiwa kuacha lindo na kutinga ukumbi wa
disko wakiwa na silaha nzito za kivita aina ya SMG.
Tukio hilo lilitokea usiku wa Aprili 20 mwaka huu, ambapo askari hao
zaidi ya watano waliingia katika ukumbi wa disko wa High Way uliopo njia
panda ya Himo na hivyo kutoa mwanya kwa magari sita aina ya Fuso
yaliyokuwa yamesheheni sukari ya magendo kupita kirahisi kwenda nchini
Kenya.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima umebaini kuwa baada ya askari
hao kutinga katika ukumbi huo, ilichukua muda wa dakika 20 magari
yakaanza kupita eneo hilo ambako askari hao walikuwa wameweka doria
katika barabara ya Mwika.
Mbali na askari hao, pia maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
nao huweka doria katika barabara hiyo ya Mwika, lakini siku hiyo
waliungana na askari wale katika ukumbi wa disko na kuacha magari hayo
yakienda Kenya bila kukaguliwa.
Hata hivyo, raia wema waliwasiliana na waandishi wa habari za
uchunguzi ambapo magari mawili yalijikuta mikononi mwa wananchi huku
moja likiwaponyoka baada ya dereva wake kukimbia na kwenda kulificha
katika mji mdogo wa Himo.
Gari lililobaki mikononi mwa wananchi wakiwamo pia waandishi wa
habari za uchunguzi lilikuwa na namba za usajili T 695 BXH aina ya Fuso
mali ya Susan Bahati Paul wa Moshi Mjini ambalo lilibainika kusheheni
sukari kutoka nchini Thailand.
Gari hilo ambalo lilikuwa mita chache kuingia nchini Kenya kupitia
eneo la machimbo ya mchanga aina ya pozolana, lilikabidhiwa kwa maofisa
wa TRA katika kituo cha forodha cha Holili likiwa na mifuko 250 ya
sukari yenye ujazo wa kilo 50 kia moja.
Alipoulizwa jana juu ya askari wake kwenda kustarehe disko na kuacha
sukari ikienda Kenya, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Koka
Moita pamoja na kudai hana taarifa, aliahidi kulishughulikia suala
hilo.
Wakati Moita akidai hana taarifa, habari za ndani ya Jeshi la Polisi
zimedokeza kuwa askari wote waliokuwa zamu mpakani hapo usiku wa kuamkia
Aprili 20 mwaka huu, wamehojiwa juu ya tuhuma za kuachia magari hayo
yaliyosheheni sukari ya magendo.
Taarifa hizo zimedokeza kuwa askari hao waliokuwa kwenye magari
mawili ya FFU, waliitwa na kuhojiwa ofisini kwa mkuu wa upelelezi wa
makosa ya jinai Mkoa wa Kilimanjaro (RCO), Ramadhan Ng’anzi.
Zaidi ya magari kumi aina ya Fuso yaliyosheheni sukari ya magendo
yamekuwa yakivuka mpaka kwenda nchini Kenya kila siku kutoka katika mji
mdogo wa Himo kupitia njia ya Kwa Hussein hadi yalipo machimbo ya
mchanga aina ya pozolana mita chache kutoka kituo cha forodha cha
Holili na kuingia nchini Kenya kirahisi.
No comments:
Post a Comment