SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, amepata
wakati mgumu kuwashawishi wabunge wakubali mabadiliko ya kanuni mpya
zitakazotumika wakati wa mjadala wa bajeti.
Hali
hiyo ilitokea jana ndani ya Ukumbi wa Pius Msekwa ambapo wabunge wote
walikutana pamoja na mambo mengine kupitia mabadiliko ya kanuni zitakazotumika
kwa ajili ya utaratibu mpya wa kupitisha bajeti.
Habari
kutoka ndani ya kikao hicho, zilisema kuwa kanuni iliyopingwa na wabunge wengi,
hasa wa Chama Cha Mapinduzi ni ile iliyotaka majina ya wachangiaji wa
mijadala ya bajeti za wizara mbalimbali yapitie na kuteuliwa kwenye vyama vyao.
Kanuni
hiyo ni tofauti na ya sasa ambapo majina ya wabunge wanaotaka kuchangia,
hupelekwa kwa Spika moja kwa moja na wabunge wenyewe na ndiye anayeteua majina
ya wachangiaji.
Kwa
mujibu wa habari hizo, idadi kubwa ya wabunge waliopinga ni wa CCM, ambao
walidai kuwa utaratibu huo utakuwa na upendeleo, kwani viongozi watakaoletewa
majina hayo wanaweza wasiyateua kutokana na tofauti miongoni mwao.
Mbunge
machachari mwingie ambaye amewahi kuitwa mara kadhaa na viongozi wa chama chake
na kumtaka aache kuishambulia serikali, alisema kuwa utaratibu huo utamnyima
haki ya kuchangia bungeni kwani anaamini hata viongozi wa CCM walio nje ya
Bunge, wataingilia kati kutaka asipewe nafasi. Mbunge huyo ambaye jina lake
tunalihifadhi, alimtaka Spika kuacha kukwepa majukumu yake.
Endapo
kanuni hiyo itapita, itaanza kutumika leo baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
kusoma hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Kabla
ya Pinda kuwasilisha bajeti ya ofisi yake, wabunge wanatarajiwa kupitisha
mabadiliko machache ya kanuni na huenda kukawa na mvutano wa kupitisha kanuni
hizo.
Bunge
litaanza kupitia na kujadili hotuba za bajeti za wizara mbalimbali ambapo mwaka
huu zitaanza wizara kabla ya kusomwa kwa bajeti ya serikali.
Katika
hatua nyingine, Spika wa Bunge, Makinda, amefuta kesi ya wabunge wa CHADEMA
waliodaiwa kufanya vurugu katika mkutano wa 10 wa Bunge mjini Dodoma.
Spika
aliwataka wabunge hao kusahau yaliyopita na kuanza moja, kwani lengo la wabunge
ni kuwatumikia wananchi waliowachagua.
Habari
kutoka ndani ya kikao hicho, zilisema kuwa baadhi ya wabunge wa CHADEMA
walimwonya Spika kuwa kama ataendelea na staili yake ya kuwabana wapinzani na
kukiuka kanuni hawatavumilia.
CHANZO: TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment