FILAMU mpya ya nguli wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba,
inayojulikana kwa jina la ‘Love and Power’ itaanza kusambazwa kuanzia
Aprili 12 mwaka huu.
Filamu hiyo iliyozinduliwa Aprili 7 katika viwanja vya Leaders jijini
Dar es Salaam ikiendana na maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kufariki
dunia kwa nguli huyo, tayari imeanza kuwa gumzo kubwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa filamu hiyo, mdogo wa Kanumba, Seth
Bosco, ambaye ni msimamizi wa Kampuni ya Kanumba The Great, aliwashukuru
Watanzania waliokuwa wamejitokeza.
Alisema siku ya juzi hawezi kuisahau katika maisha yake kutokana na
kuzinduliwa kwa kazi ya kimataifa iliyofanywa na Kanumba kabla ya
kufariki dunia Aprili 7, mwaka jana.
“Kanumba alikuwa na ndoto za kuikomboa nchi yetu katika tasnia ya
filamu, nafikiri naye Mungu anajua ni kwanini kamchukua, hivyo yatupasa
kushukuru kwa kila jambo,” alisema Bosco.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wasanii nyota kutoka Ghana, Ama Abebrese,
Ama Mc Brown na aliyekuwa Meneja wake wa Kimataifa, Prince Richard na
wasanii mbalimbali wa filamu wa hapa nchini.
Kanumba alifariki dunia Aprili 7, mwaka jana nyumbani kwake Sinza –
Vatican jijini Dar es Salaam, huku kifo chake kikihusishwa na msanii
mwenzake, Elizabeth Michael ‘Lulu’.
No comments:
Post a Comment