WANAJESHI nchini wametakiwa kuacha kujichukulia sheria mikononi
na kuwapiga raia zinapotokea vurugu kwani kwa kufanya hivyo ni
kusababisha uvunjifu wa amani.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, alipokuwa akijibu swali
kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria.
Katika swali lake, Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM) alihoji
serikali kuhusu malalamiko yanayotolewa mara kwa mara na wananchi
yanayotokana na vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na wanajeshi
katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na kuwapiga wananchi.
“Pia yamekuwapo malalamiko kutoka kwa raia ambao wamekuwa wakivaa
mavazi ya jeshi na kujifanya kuwa wao ni wanajeshi na kutumia mwanya huo
kufanya vitendo vya uhalifu, hivyo kulichafua jeshi letu ambalo
limekuwa likifanya kazi kubwa ya ulinzi na usalama wa nchi hii ya
Tanzania,” alisema Bulaya.
Akiendelea kujibu swali hilo, Waziri Kombani alisema ni kweli kwamba
kumekuwapo na malalamiko ya askari kuwapiga raia mara zinapotokea
vurugu.
Akizungumzia baadhi ya watu kutumia mavazi ya jeshi kufanya uhalifu,
alisema ni kweli watu wa aina hiyo wapo, lakini serikali imekuwa
ikiendelea kufuatilia na kuwachukua hatua stahiki wale wanaobainika
kutenda makosa hayo.
Katika swali jingine la nyongeza, Mbunge wa Mkanyageni, Injinia
Habibu Mnyaa (CUF), ameihoji serikali kama iko tayari kufanya utaratibu
wa kumlipa fidia mtu anayewekwa mahabusu bila hatia mara anapoachiwa
huru na kugundulika kuwa hana hatia.
Akijibu swali hilo, Waziri Kombani alisema serikali haina utaratibu
wala sheria yoyote ya kumlipa fidia mtu aliyewekwa ndani na kutolewa
baada ya kugundulika kuwa hana hatia.
Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu, Fakharia Shomar
Khamis (CCM), alihoji serikali ina utaratibu gani wa kumsaidia au
kumlipa fidia muathirika ambaye alikuwa nyumbani kwake, kwa bahati mbaya
akapata athari ya mali yake au kuumia inapotokea hali ya uunjifu wa
amani.
Akijibu swali hilo, Kombani alisema kwa utaratibu wa sheria zilizopo,
serikali haina utaratibu wa kumlipa fidia muathirika yeyote wa madhara
ya uvunjifu wa amani pale inapothibitika kusababishwa na mtu au watu
binafsi.
No comments:
Post a Comment