JESHI la Polisi Mkoa wa Temeke jijini Dar es Salaam limeingia
katika kashfa ya kuwalazimisha ndugu wa mtuhumiwa aliyefia mikononi
mwao watoe fedha za kununulia mafuta ya sh 40,000 kwa ajili ya
kusafirisha mwili wa marehemu kwenda kuufanyia uchunguzi.
Tanzania Daima lilidokezwa jana kuwa ndugu hao walifika Kituo cha
Polisi Temeke juzi kwa ajili ya kuomba mwili wa marehemu ufanyiwe
uchunguzi kufuatia kifo chake kutawaliwa na utata, huku watuhumiwa wa
mauaji hayo nao wakiwa bado hawajakamatwa.
Katika sakata hilo, ndugu wa marehemu Gasper Augustino Mlay,
wanalituhumu jeshi hilo Mkoa wa Temeke kwa kumpiga na kumsababishia kifo
mpangaji huyo aliyeshindwa kuhama kwa muda aliopangiwa na mwenye
nyumba wake, Aprili 13, mwaka huu.
Wakizungumza na gazeti hili, ndugu wa marehemu, Peter Masoy na
Elizabeth Mlay, walisema kuwa Gasper alikuwa amepewa notisi ya kuhama
ndani ya siku 30 lakini hakuweza kufanya hivyo kwani hadi siku ya tukio
alikuwa bado anasubiri kupata fedha.
Waliongeza kuwa siku hiyo mwenye nyumba alifika kumhamisha ndugu yao
akimwamuru atoke, yapata saa 12 asubuhi, lakini alikataa, akaomba
kupambazuke, hivyo akajifungia ndani.
“Kitendo hicho kilimfanya mwenye nyumba kumwita mjumbe wa mtaa huo,
wakaenda polisi, wakarejea katika nyumba hiyo wakavunja mlango na
kumpiga hadi alipozidiwa ndipo wakamchukua kumpeleka Kituo Kidogo cha
Polisi Sandali.
“Lakini wakiwa njiani Gasper aliwaomba awapatie namba za simu ili
waweze kutuita ndugu kwa ajili kumdhamini. Mwenye nyumba na askari huyo
walikubali kutupigia na tukafika,” walisema.
Waliongeza kuwa mdogo wa marehemu Elias Mlay alipelekwa hadi
alipokuwa akipanga kaka yake ili kukagua uharibifu uliosababishwa na
ndugu yao.
“Kwa kuwa uharibifu haukuwa mkubwa, hivyo aliomba kulipa sh 20,000
kwa askari Moses Zimba ili wayamalize badala ya sh 300,000.
“Lakini tulipokwenda kituoni ili kumwona ndugu yetu na kumdhamini,
tulikuta amefariki dunia huku akiwa na uvimbe mkubwa tumboni. Tulipeleka
taarifa Kituo cha Polisi Chang’ombe ambao walitoa gari na kuja
kuchukua mwili wa marehemu kuupeleka Hospitali ya Temeke,” walisema.
Ndugu hao waliongeza kuwa polisi waliwaambia kwamba walikuwa
wamechelewa hivyo kuwataka warudi jana kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi
mwili huo.
“Tulipofika kituoni tuliambiwa kuwa uchunguzi huo hautafanyika hapa
Hospitali ya Temeke bali Hospitali ya Taifa Muhimbili lakini kwanza
tukatakiwa tulipe sh 40,000 kwa ajili ya mafuta ya gari,” walisema.
Walifafanua kuwa walielezwa kwamba Hospitali ya Temeke hairuhusiwi
kufanya uchunguzi wa mwili wa ndugu yao kwa kuwa ulikuwa na utata sana.
Kutokana na mkanganyiko huo, gazeti hili lilimtafuta Mganga Mkuu wa
Hospitali ya Temeke, ambaye naye alielekeza Katibu Tawala wa hospitali
hiyo aweze kufafanua kuhusu suala la uchunguzi wa mwili.
Katibu huyo alisema Hospitali ya Temeke ni ya mkoa hivyo hutoa huduma
za uchunguzi, hivyo mwili wa marehemu Gasper haukuwa na sababu ya
kupelekwa Muhimbili.
Alipotafutwa kufafanua juu ya sakata hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa
wa Temeke, Englibert Kiondo, alikiri kuwa magari ya polisi hayakuwa na
mafuta, lakini akasema si kitendo kizuri kwa askari kuomba mafuta
kutoka kwa ndugu wa marehemu.
Kamanda Kiondo aliagiza mwili huo uchunguzwe huku akiwahakikishia
ndugu wa marehemu kuwa watuhumiwa wa mauaji hayo, yaani mwenye nyumba
pamoja na mtu aliyetambulishwa kama polisi shirikishi tayari
wanashikiliwa na polisi.
Hata hivyo, taarifa zaidi zimesema kuwa ndugu wa marehemu walikuwa
wakishinikizwa na polisi kuuchukua mwili huo kwa kisingizio kuwa
marehemu alifariki dunia kwa kudhuriwa na moshi uliotokana na nyumba
kuwaka.
Alipotafutwa kwa simu mtuhumiwa wa mauaji hayo anayetajwa kuwa ni
askari, alikiri kupatwa na tatizo hilo lakini akamuomba mwandishi
waonane ana kwa ana wayamalize kabla ya kukamatwa.
Katika hatua iliyoonesha kuwapo kwa mkanganyiko mkubwa, Kamanda
Kiondo aliwasiliana na mwandishi wa gazeti hili na kumwita ofisini
kwake, lakini alipofika alimwelekeza akaonane na Mkuu wa Upelelezi ili
asome faili na kuangalia fomu ya uchunguzi.
Alitamba kuwa uchunguzi wa mwili wa marehemu ulikuwa umefanyika, jambo ambalo halikuwa la kweli.
Gazeti hili kama lilivyoelekezwa na Kiondo lilifika ofisini kwa Mkuu
wa Upelelezi ambaye naye aliomba asubiriwe kwani alikuwa na wageni.
Wakati mwandishi akisubiri nje, alipigiwa simu na Kamanda Kiondo
lakini kwa kutumia simu tofauti akimuuliza: “Hivi wewe ndiye umesema
unatoka CHADEMA?” Alipojitambulisha kuwa ni mwandishi wa habari,
Kamanda Kiondo akakata simu.
Baadaye kamanda huyo alimpigia simu mwandishi na ndugu wa marehemu
pamoja na aliyekuwa askari aliyekuwa akipeleleza tukio hilo ili akutane
nao ofisini.
Hata hivyo baada ya ndugu wa marehemu kusema tayari wameleta fedha
waliyoombwa kwa ajili ya mafuta, polisi waligeuka wakidai: “Mlisikia
vibaya, sisi mafuta tumeshaleta, ni mara nyingi tunajitolea fedha zetu
za mfukoni kuweka mafuta kwenye magari.”
No comments:
Post a Comment