VIONGOZI wa Kata ya Wazo, Dar es Salaam, wamedaiwa kuchakachua
uchaguzi wa Baraza la Katiba kwa kuweka wajumbe bila kupigiwa kura.
Wakizungumza na Tanzania Daima jana, wajumbe waliochaguliwa ngazi ya
mtaa ambao walitakiwa kufanyiwa uchaguzi ngazi ya kata, walisema siku ya
uchaguzi walisubiri katika eneo la ofisi, lakini uchaguzi haukufanyika
na badala yake mmoja wa wenyeviti wa mtaa alikwenda kwa wajumbe
wanaosubiri uchaguzi na kuwaambia kuwa uchaguzi umefanyika na watu
wameshapatikana.
Mmoja wa wajumbe hao, Gration Mbelwa, alisema taarifa ya mwenyekiti
huyo iliwashitua na kuondoka katika eneo hilo huku wakijua viongozi wa
kata wameafanya hujuma na kuteua watu wao.
Mbelwa alisema baada ya kuona zoezi hilo limepita katika mazingira
tata, wameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
kuchunguza tukio hilo na Manispaa ya Kinondoni kurudia uchaguzi.
Alisema viongozi wa Kata ya Wazo wamekiuka taratibu za uchagazi wa
mabaraza uliotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya na kwamba
hawana imani na viongozi hao.
Christina Komba alisema viongozi wa Kata ya Wazo si waaminifu, hivyo hawaoni umuhimu wao.
Mratibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Ali Saadat, alisema watu
ambao wamepitishwa bila kufuata sheria na kanuni zilizowekwa, tume
haitawatambua.
“Kama kuna watu wamepitishwa bila ya kufanyika uchaguzi, tume
haitapokea majina hayo, wanachotakiwa ni watu kupatikana kupitia
uchaguzi,” alisema.
No comments:
Post a Comment