Katika
gazeti la Mtanzania toleo na. 7269 la Jumatano Machi 27, 2013 kuna habari yenye
kichwa chenye maneno ‘SIRI YA KUUWAWA ZITTO YAFICHUKA’ na vichwa vidogo
‘yadaiwa ilipangwa anyweshwe sumu hotelini’ Dk. Slaa atajwa kumtuma Saanane
kummaliza’.
Habari hii imeniletea usumbufu mkubwa kwani ndugu, jamaa, marafiki na wapiga kura wangu, wamejazwa na wasiwasi mkubwa sana kwamba ninaweza kuuwawa.
Napenda
kusema yafuatayo:
Moja,
sijawahi katika maisha yangu yote kukutana na mtu anayeitwa Ben Saanane na
hivyo hicho kikao ambacho inasemekana nilikuwa naye na akajaribu kunipa sumu
hakijawahi kutokea.
Imetajwa Hoteli ya Lunch Time ambayo sio tu sijawahi kufika,
pia hata siijui ipo wapi. Haijawahi kutokea mimi kufanya kikao cha pamoja na
Ben Saanane, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba. Hivyo habari iliyoandikwa ni ya
kufikirika na hivyo naomba mwandishi ahakikishe kuwa vyanzo vyake vya habari
vimempa habari sahihi.
Pili,
Siamini kamwe kuwa Katibu Mkuu wa chama changu anaweza kupanga kuniua maana
hana sababu ya kufanya hivyo. Napenda kurudia kusema kwamba mimi ninaamini kuwa
kila nafsi itaonja mauti. Kila mtu atakufa. Kama nitakufa kwa kuuwawa na mtu
mwingine ndio itakuwa nimeandikiwa hivyo na Mungu.
Ndio maana hata siku moja
silalamiki kuhusu vitisho vya kuuwawa nk. Kama kuna mtu anafikiria kuwa kumuua
Zitto ndio furaha ya maisha yake atakuwa anajidanganya tu maana Zitto anaweza
kufa kimwili lakini mawazo, fikra na maono ya Zitto yataishi tu.
Siogopi kufa
maana maisha niliyoyachagua ndio haya ambayo yamejaa vitisho. Muhimu kwangu ni
kufanya kazi zangu kwa bidii, uhodari na uaminifu. Siku zote nitasimamia ukweli
bila kujali uchungu wa ukweli huo.
Tatu,
nawashauri watu ambao wamehama CHADEMA na kuhamia vyama vingine watumie muda
wao kujenga vyama vyao badala ya kila siku kuzungumzia masuala ya chama ambacho
wao sio wanachama tena. Kama mtu kaamua kuhama CHADEMA anapoteza haki ya
kujadili masuala ya CHADEMA maana kama angekuwa anapenda kuyajadili asingehama.
Mh. Zitto Z Kabwe |
Naonya mtu yeyote ambaye anatumia jina langu ili kufanikisha malengo yake ya
kisiasa. CHADEMA sio pango la watesaji wala wauaji. Kama kuna mwanachama wa
chama kingine cha siasa anayedhani kuna mtu ndani ya CHADEMA anapanga mipango
ovu aende kwenye vyombo vya sheria kumshtaki. Matendo ya mtu mmoja yasifanyiwe
propaganda kama ni malengo ya taasisi.
Nne,
Nawashauri viongozi wenzangu wa CHADEMA na hasa wanachama tutumie muda wetu
kujenga mshikamano ndani ya chama. Fitna, majungu, uongo, uzandiki nk kamwe
havijengi chama.
Chama chetu lazima kiwe mfano bora wa kuheshimu demokrasia na
haki za binaadamu. Wananchi hawawezi kutoa dola kwa chama chenye mifarakano.
Tusiruhusu kugawanywa kwa matakwa ya watu wachache. Tusimamie misingi ya
kuanzishwa chama chetu.
Imetolewa na
Naibu Katibu Mkuu CHADEMA Tanzania Bara,
Mh. Zitto Z Kabwe.
No comments:
Post a Comment