Katika taarifa kwa taifa, makamu wa rais wa
Venezuela Nicholas Marduro ametangaza kufariki dunia kwa rais Hugo
Chavez, 58, kufuatia kuugua muda mrefu maradhi ya Saratani. Rais Chavez
ametoweka katika hadhira ya nchi hiyo kwa muda mrefu ambapo alikuwa
anapokea matibabu nchi jirani ya Cuba.
Alirejea , mjini Caracas mnamo Februari 18 kwa
mara ya kwanza tangu maradhi yake yamzidie ambapo alipelekwa hospitali
ya kijeshi kuendelea kupokea matibau. Hata hivyo maelezo zaidi
hayakutolewa juu ya afya yake. Waandamanaji waliandamana katika mji mkuu
Caracas mwishoni mwa juma wakidai kuwa watu wa Venezuela wanapaswa
kupewa habari zaidi kuhusu afya ya rais wao.
Bwana Chavez amekua uongozini nchini
Venezuela kwa miaka 14 na anatazamiwa kuleta mageuzi makubwa
yaliyolenga zaidi kuimarisha maisha ya raia wa pato la chini.
Ujumbe wa Jeshi
Taarifa kutoka kwa jeshi imesema kuwa
wataendelea kuilinda hadhi ya nchi na kuimarisha usalama. Pia jeshi
limeahidi kuendelea kuwa waaminifu kwa makamu wa rais Nicholas Marduro
na wakatoa wito kwa raia kuwa watulivu.
Chavez - wasifu
Hugo Chavez alijitosa katika siasa za Venezuela mnamo Februari 1992 akiwa luteni katika jeshi. Aliongoza mapinduzi dhidi ya rais wa wakati huo Carlos Andres Perez.
Lakini kutokana na kukosa usaidizi wa kutosha wa kijeshi, Chavez na wanamgambo wenzake walishindwa kunyakua madaraka hayo. Alikiri kushindwa na aliwekwa korokoroni.
Aliingia uongozini baada ya ushindi mkubwa
ulioviondosha vyama vya kisiasa wakati huo. Katika kuapishwa kwake mnamo
February 1999, Hugo Chavez alitangaza wazi kwamba mipango yake ya
mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi sio kampeni tu. Alitimiza ahadi yake
na kuiongoza nchi hiyo katika mabadiliko ambayo hayakuwahi kushuhudiwa
katika muda wa miongo kadhaa. Alibadili muundo wa bunge na kulifanya
kuwa la kikatiba, ambalo liliiunda katiba mpya baada ya kura ya maoni
iliyoidhinishwa na 88% ya wapiga kura.
Rais Chavez alitaifisha rasilmali ukiwemo
utajiri wake mkubwa wa mafuta. Sera kama hizi zilimfanya azozane na
kampuni za kimataifa za mafuta, lakini alipata uungwaji mkono mkubwa wa
watu maskini.
Kutokana na urafiki wake na viongozi wa mrengo
wa kushoto kama vile rais wa Cuba, Fidel Castro, ambaye walikuwa na
uhusiano wa karibu aligongana kidiplomasia na Marekani, ambayo ni
mshirika wake mkuu wa kibiashara.
Chavez alipendwa nyumbani na wafuasi wake lakini
alipingwa na baadhi ya watu nchini humo na katika nchi za nje.
Alionekana sio tu kama bingwa wa jamii maskini lakini pia kama
muingiliaji wa siasa za nchi jirani. Katika miaka ya hivi karibuni
alilenga kukabiliana na masuala ya ndani ya Venezuela, kama uhalifu,
kuinua uchumi wa nchi na kukabiliana na rushwa.
No comments:
Post a Comment