KUFUNGASHWA virago kwa timu
ya Simba kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kumeweka kwenye wakati
mgumu wachezaji wakongwe wa timu hiyo, imefahamika.
Juzi, Simba iliaga michuano
hiyo katika hatua ya awali baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-0; ilinyukwa 1-0 kwenye
Uwanja wa Taifa wiki mbili zilizopita kabla ya kulimwa 4-0 waliporudiana
mjini Libolo.
Habari kutoka ndani ya klabu
ya Simba, zinasema uongozi umedhamiria kuwaondoa wakongwe hao kundini kwani
ndio chachu ya timu kupata matokeo yasiyoridhisha katika michezo yake ya hivi
karibuni.
Katika kikao cha dharula cha
kamati ya utendaji ya Simba wiki iliyopita kilichoitishwa kwa ajili ya kujadili
mwenendo mbovu wa timu hiyo katika siku za hivi karibuni, ilibainika wakongwe ni
moja ya sababu.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa,
wakongwe hao wamekuwa wakieneza ‘virusi’ vibaya kwa chipukizi, hivyo kuathiri
ufanisi wa timu hiyo dimbani, hivyo uongozi unakuzudia kuchukua uamuzi mgumu
kwa maslahi ya timu hiyo.
Kilisema kutokana na uongozi
kuchoshwa na hali hiyo, umeona ni heri kuwaondoa kundini watovu wote wa nidhamu
ili kutoa nafasi yaw engine kusajiliwa ambao watashirikiana na wengine wenye
nidhamu waliopo kwenye timu hiyo na kusema katika hilo hawatajali umaarufu wa
mchezaji.
“Hatutaaangalia sura, uzoefu wala kiwango,
tutawafyeka wote wanaoleta haya matatizo na uamuzi huo tutaanza kuutekeleza
hivi karibuni,” alisema kiongozi huo bila kutaja wachezaji wanaodaiwa kueneza
virusi katika timu hiyo.
Hata hivyo, baada ya kikao hicho
ambapo pamoja na mambo mengine kiliazimia kuitisha mkutano mkuu wa dharula wa
wanachama, wachezaji kwa upande wao walikutana
na kamati ya ufundi na kueleza wamekuwa wakikwazwa na mmoja ya makocha
na baadhi ya viongozi.
Wacheza walikwenda mbali na
kufichua kufanya vibaya kwa timu hiyo, si bahati mbaya isipokuwa kufikisha
ujumbe wa kuwakataa kocha huyo na baadhi ya viongozi kwa kuwapendelea baadhi ya
wachezaji wakati wachezaji wote wanapaswa kupewa haki sawa ndani ya timu.
Mbali ya kung’olewa kwenye michuano
ya kimataifa, Simba pia imekuwa na mwendo mbaya kwenye kampeni za kutetea
ubingwa wa Ligi Kuu ikishika nafasi ya tatu kwa pointi 31, ikitanguliwa na
kinara Yanga yenye pointi 42 na Azam ya pili kwa pointi 36.
Novemba mwaka jana, uongozi
wa klabu hiyo chini ya Mwenyekiti wake Ismail Aden Rage, ulimtimua aliyekuwa
kocha mkuu Mserbia, Milovan Cirkovic kwa kile kilichoelezwa kufanya vibaya kwa
timu hiyo baada ya kumaliza raundi ya kwanza ya Ligi Kuu ikiwa nafasi ya tatu.
Nafasi yake ikazibwa na
Mfaransa Patrick Liewig, akisadiwa na Jamhuri Kihwelo huku kocha wa makipa
akiwa James Kisaka na Meneja ni Mosea Basena.
No comments:
Post a Comment