Saturday, March 2, 2013

MTOTO AOKOTWA POLINI AKIWA HAI

Mtoto mmoja jinsia ya kiume amenusurika kifo wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe baada ya kuzaliwa na kutupwa porini na mama yake jirani na makazi ya watu na kuokotwa na raia wema ambapo walimuwaisha hospitari ili kuokoa maisha yake.

Akionge na waandishi wa habari Muuguzi wa zamu katika hospitari ya wilaya ya Ludewa Bi.Eda Muhema alisema alimpokea mtoto huyo kutoka kwa wasamalia wema waliotokea Ludewa Kijijini mtaa wa songambele majira ya jioni Februal 28 mwaka huu akiwa katika hali nzuri kutokana na wasamaria hao kumsitiri kwa nguo nzito.

Bi.Muhema alisema mtoto huyo aliletwa akiwa na uzito wa kilo tatu na akiwa ameshakatwa kitovu kwa kutumia panga hivyo alichokifanya yeye ni kukipunguza kitovu hicho na kumtengeneza kitaalamu zaidi.

“tumempokea akiwa salama kama mnavyomuona lakini inaonekana amezaliwa usiku na kapigwa na baridi lakini kutokana na umahili wa akinamama waliomuokota waliweza kumpa huduma ya kwanza na kufunika nguo nzito ili kumsaidia kurudisha joto lake la mwili,”alisema Bi.Muhema.

Kwa mujibu wa shuhuda mmoja wa tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Mrs.Kidulile ambaye ni muuguzi mstaafu alisema ilikuwa ni majira ya jioni februal 28 mwaka huu aliona wanafunzi wakishangaa kitu katika shamba la mahindi.

Ndio alipowauliza kunani hapo nao wakamjibu kuwa kuna kitoto kichanga kimetupwa hapa alisema kutokana na taaluma yake alifika eneo la tukio na kubaini kuwa mtoto huyo alikuwa bado yuko hai,akawaita wanawake wazie na kuchukua nguo ili kumfunika.

Mrs.Kidulile alisema mtoto huyo alitupwa jirani na makazi ya watu ambapo palikuwa na maji yakitiririka kutoka katika bomba lililo pasuka lakini maji hayo hayakuweza kumfikia alipolazwa.

Alisema walimkuta mtoto huyo akiwa hajakatwa kitovu na akiwa kaviringishwa katika gunia hivyo walilazimika kumkata kitovu kwa kutumia panga alilobeba mama mmoja aliyekuwa akienda shambani na kumuwahisha hospitali ili ahifadhiwe vizuri.

 Katika kuulizia kwa wajirani ndipo walipompata mwanamke aliyemtupa huyo mtoto wakamchukua na kumfikisha katika kituo hicho cha polisi cha Ludewa mjini ambako mwnamke huyo anaendelea kushikiliwa na jeshi la Polisi.

Aidha mama huyo Bi.Magdarena Lugongo anayetuhumiwa kwa kosa la kumzaa mtoto na kumtupa akihojiwa na waandishi wa habari alikili kutenda kosa hilo na kueleza sababu kubwa ni ugomvi ndani ya ndowa.

Bi.Magdarena alisema alifanya uamuzi huo kutokana na hasira kwani mumewake aliye mtaja kwa jina la Andrea Kayombo aliukataa ujauzito huo kuwa sio wake na kumpa manyanyaso makubwa pindi anaujauzito.

Alisema ujauzito huo ni wa sita lakini alimshangaa mumewe kwa kuukana ndio alipopatwa na uchungu wa kujifungua hakutaka msaada kwa mtu yeyote akajifungua peke yake majira ya usiku na ilipofika alfajiri aliamua kumtelekeza mtoto huyo jirani na makazi ya watu.

Bi.Magdarena aliamuliwa na jeshi la polisi akiwa chini ya ulinzi kumnyonyeha mtoto huyo naye alikubari kufanya hivyo na kuomba aitwe mumewe ili waweze kuliweka sawa jambo hilo la nani muhusika wa ujauzito lililopelekea mtoto huyo kutupwa.

Na Nickson Mahundi Ludewa

No comments:

Post a Comment