MWANAFUNZI wa darasa la sita katika Shule ya Msingi ya Kasumulu,
kata ya Ngana, wilayani Kyela, Kaselema Mpale (14), ameuawa kikatili
kwa kuchinjwa na kisha kunyofolewa baadhi ya viungo sehemu ya mwili
wake.
Akizungumza na Tanzania Daima juzi, mama wa mtoto huyo, Lucia
Kamnyonge, alisema kuwa tukio hilo lilitokea Ijumaa saa 10:30 akiwa
ametumwa na baba yake kwenda nyumba ya jirani kuchukua mpunga ambao
ungetumika kama chakula cha siku hiyo.
Alisema kuwa toka siku hiyo hakupatikana hadi alipokutwa kesho yake
akiwa amekufa kwa kuchinjwa na kisu na kunyofolewa baadhi ya sehemu zake
za mwili kama pua, mdomo, jicho, sehemu zake za siri na kuchunwa ngozi
ya kichwa karibu na utosi na mwili wake kutundikwa juu ya mti.
Alisema kuwa baada ya kutoonekana, taarifa ilipelekwa kwenye ofisi ya
serikali ya kijiji ambapo uliitishwa mkutano wa wananchi wote wa kijiji
hicho na kuanza kumtafuta mtoto huyo bila ya mafanikio.
Baadaye baba yake alikuta mwili wake juu ya mti ukiwa umetundikwa
kichwa chini miguu juu na viungo vyake hivyo vikiwa vimenyofolewa.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Ibungumbati, kijiji cha Ushirika, Adamu
Mkese, alisema kuwa tukio hilo limewashtua wananchi wa eneo hilo na
kwamba katika mkutano wa dharura wa kijiji, wananchi walimhusisha baba
wa mtoto huyo, Mpale Mbisa (35), katika mauaji hayo.
Alisema kuwa wanakijiji walitilia shaka kutokana na mazingira ya kifo
chenyewe na maelezo ya kujichanganya aliyoyatoa baba huyo hasa jinsi
alivyomkuta mtoto huyo akiwa amekufa katika eneo ambalo wananchi
walipita usiku na mchana wakimtafuta bila kumuona.
Wananchi walimtuhumu baba huyo kuwa alichukua fedha sh milioni saba
ili kumuuza mtoto wake. Tuhuma hizo zilililazimu Jeshi la Polisi
kumkamata mzazi kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Naye ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Naomi Charles, alisema kuna
dalili zote za baba huyo kuhusika katika mauaji hayo kutokana na
mazingira.
Alisema hisia hizo za wananchi zinaweza kuwa na ukweli ndani yake na
kuwa Jeshi la Polisi inabidi lifanye uchunguzi wa kina na kuwa kama
ataachiwa usalama wake utakua mdogo pale kijijini.
Ofisa tarafa ya Unyakyusa, Lwitiko Mwakalukwa, alithibitisha kutokea
kwa tukio hilo na kwamba yeye pamoja na mkuu wa wilaya walifika eneo la
tukio na kujionea unyama huo.
No comments:
Post a Comment