Monday, February 11, 2013

DC AAMURU MWENYEKITI WA CCM AKAMATWE


Mkuu wa  Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo, ameamuru kukamatwa kwa Mwenyekiti wa  Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Veli, kwa tuhuma za kuhusika na upotevu wa mashine ya mradi wa josho la ng’ombe lililopo Kata ya Mashewa wilayani hapa.

Aidha, Mkuu  huyo wa Wilaya ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, kuchunguza tuhuma  za wakala wa pembejeo za kilimo anayedaiwa kuwasambazia wakulima mbegu mbovu na kuwasababishia hasara na njaa.

Alitoa maagizo hayo wakati wa kikao cha Maendeleo ya Kata ya Mashewa (WDC) baada ya kupokea malalamiko ya mwenyekiti huyo kudaiwa kuchukua kinyemela mashine hiyo na kupeleka kusikofahamika. Ilidaiwa kuwa Veli, alichukua mashine hiyo na kuipeleka kusikojulikana na hivyo kukwamisha shughuli za utabibu wa mifugo.

Kitendo hicho kilimfanya Mkuu wa Wilaya kulitaka Jeshi la Polisi kumkamata mara moja na kumfikisha mahakamani. “Mkuu wa kituo, mtu huyo ni lazima akamatwe mara moja tena kiongozi, kwanini mpaka leo hajakamatwa!?...hao ndiyo mimi ninaowataka wawe mfano. OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya), hakikisha hilo linatekelezwa,” alisisitiza Gambo.

 Wakati Mkuu huyo wa Wilaya akitoa maagizo hayo,  viongozi hao ambao walikuwapo kwenye  kikao hicho kilichofanyika mwishoni mwa wiki katika Shule ya Msingi Mashewa.

Mkuu huyo wa Wilaya alilazimika kuliagiza Jeshi la Polisi kumkamata  Mwenyekiti huyo wa CCM tawi la Mtonibombo, kufuatia taarifa ya kata iliyosomwa mbele yake ambapo pamoja na mambo mengine, ilimlalamikia Veli, kwa madai ya kuchukua mashine ya josho hilo na kusababisha mifugo kukosa matibabu na hivyo kuathiriwa na magonjwa mbalimbali.

Gambo aliyefuatana na kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya, alikerwa na taarifa hiyo na kushangaa kwanini hajakamatwa licha ya taarifa hizo kufikishwa polisi.

“Hivi nauliza, ninyi polisi mna ajenda gani na Veli? au kwa kuwa ni Mwenyekiti wa CCM…hakuna hiyo sasa nataka kabla jua halijachwa, awe ameshakamatwa, sawa?,” alisisitiza.

Awali, wakitoa maelezo yao kuhusiana na tukio hilo, wajumbe wa kikao hicho, walimshutumu Veli kwamba amechukua mashine hiyo kinyemela na haifahamiki ilipo na kila alipoulizwa hudai kuwa ni mbovu ipo kwa fundi.

Hata hivyo, imedaiwa kuwa hata alipotakiwa na kamati ya mradi huo airejeshe, hakutekeleza. Walidai kuwa Veli ni mjumbe mwenzao katika kamati hiyo, hivyo hakuwa na mamlaka yoyote ya kuchukua mashine hiyo bila baraka za kikao husika, hivyo kitendo hicho kinawatia hofu kuwa inawezekana amekifanya kwa nia mbaya ya kuhujumu huduma hiyo muhimu kwa wafugaji.

Mambo mengine yaliyojitokeza katika kikao hicho ni usambazaji wa mbegu mbovu zilizotolewa na wakala wa pembejeo za kilimo ambazo zimewafanya wakulima kuingia kwenye janga la njaa baada ya kuzipanda na kushindwa kuota.

Ilidaiwa kuwa wakala huyo ambaye hakutajwa jina, alisambaza mbegu hizo kwa wakulima lakini hazikuota na walipozifanyia uchunguzi walibaini kuwa zimeisha muda wake.

Hata hivyo, Gambo katika kulizungumzia suala hilo aliuagiza uongozi wa halmashauri kulifuatilia ikiwa ni pamoja na kumchunguza aliyesambaza pembejeo hizo na kubaini kuwa nani anahusika kati ya wakala huyo na halmashauri ya wilaya.

Alisema anachotaka ni kujua kama mbegu hizo zilifika halmashauri zikiwa zimekwisha muda wake ama ziliharibika baada ya kuwasilishwa kwenye halmashauri na kama ndivyo, atambulike aliyetoa kibali cha kuzisambaza huku akijua hazifai ili achukuliwe hatua za kisheria.

No comments:

Post a Comment